Majaliwa akerwa upotevu wa fedha, atoa mfano wa milioni 500 zilizotoweka Kigoma

0
43

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema atapeleka timu maalum ya uchunguzi wilayani Kigoma ili ifanye uchunguzi wa fedha zinazopotea kinyemela kupitia mtandao wa watumishi wasio waaminifu.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na viongozi wa dini, Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenye ukumbi wa NSSF, Kigoma Mjini.

“Hapa Manispaa mnapokea fedha, zinakaa kwenye akaunti kwa muda halafu zinapotea, hazijulikani zimefanya nini. Nitaleta timu, waje wafuatilie hapa Kigoma, waende hadi TAMISEMI ili tuone huo mnyororo unaenda wapi,” amesema.

Amesema kwa kawaida fedha zinazotoka Serikali Kuu zinatumwa na maelekezo mahsusi juu ya mambo yanayokwenda kufanyika, huku za makusanyo ya ndani maamuzi ya matumizi yake ni lazima yafanywe na baraza lote la madiwani.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu amesema Manispaa ya Kigoma ilipokea TZS milioni 500 kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI zikakaa kwenye akaunti kwa muda mrefu lakini baadaye zikatoweka na hazijulikani zilitumika kufanya nini.

“Kuna watu wamejilipa TZS milioni 11 zikiwa ni posho ya safari ya Dodoma. Pia wametumia TZS milioni sita kufanya service [matengenezo] ya gari, hili ni gari la aina gani? Wengine wametumia TZS milioni 9 kwenye sherehe za Siku ya Mtoto wa Afrika na wengine wamejilipa TZS milioni 14. 8 kwenda kwenye sherehe za Nanenane Tabora, hivi mlikaa siku ngapi huko?” alihoji waziri mkuu.

Amesema kuna tume ya TAMISEMI ilikwenda kufanya uchunguzi kwenye halmashauri hiyo kuhusiana na matatizo hayo. Hivyo, ameitaka tume hiyo ikamilishe kazi yake haraka na kuiwasilisha kwa Waziri wa Nchi, OR TAMISEMI.

Send this to a friend