Majaliwa amuagiza Naibu Waziri Mkuu kushughulikia upatikanaji wa mafuta

0
38

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko kushughulikia suala la upatikanaji wa nishati ya mafuta nchini ili Watanzania wafikiwe na huduma hiyo.

Akijibu swali la Mbunge wa Lushoto, Rashid Shangazi aliyelohoji mkakati wa Serikali kuhakikisha taifa linakuwa na nishati hiyo, Waziri Mkuu amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo katika maeneo mbalimbali na kubainisha kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuleta suluhusho.

“Kufuatia mabadiliko ya Mheshimiwa Rais aliyoyafanya juzi, tumeanza kumwona Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu akifanya vikao kadhaa ndani ya wizara kukutana na wadau. Sasa kwa kuwa ameshaanza hii kazi, niendelee kumuagiza Naibu Waziri Mkuu kushughulikia hili.

Muhimu zaidi nishati yenyewe ipatikane nchini, suala la bei tunajua bei zinabadilika wakati wote lakini kwanza nishati ipatikane kwenye vituo vyote na maeneo yote nchini, ili Watanzania waipate hii huduma,” amesema.

Waziri Mkuu amesema endapo wizara zote zinazohusika, EWURA na taasisi zote za ununuaji wa mafuta zitakaa na kujadili kwa pamoja ndani ya wiki moja kuona namna ya upatikanaji wa nishati hiyo, Serikali italeta mrejesho wa kile kilichoazimiwa.

Send this to a friend