Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema katika zoezi la uokoaji wa jengo lililoporomoka katika eneo la Kariakoo mwezi Novemba, imebainika jengo hilo lilikuwa limebeba takriban robota 2,040 na viroba 10,051 vya nguo zilizokadiriwa kuwa na uzito wa tani 850 licha ya jengo hilo kuwa na uwezo wa kubeba tani 250 pekee.
Akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni kati ya Rais Samia Sauluhu na waokoaji wa Kariakoo Ikulu, Dar es Salaam amesema katika zoezi hilo la uokoaji takribani Shilingi za Kitanzania 112,886,410, Dola za Marekani 48,490, Shilingi za Kenya 6,920 na Yuan 631 zilipatikana.
“Mali hizo na fedha zote zimeendelea kurejeshwa kwa wamiliki waliotambuliwa,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, amesema baada ya Rais kumwelekeza kuunda kamati maalum ya uchunguzi wa tukio la kuporomoka kwa jengo na kufanya ukaguzi wa kina wa majengo mengine yaliyo katika eneo la Kariakoo, tayari kamati hiyo imehitimisha kazi yake na iko tayari kufanya mawasilisho kwa Rais Samia.