Majaliwa: Uwekaji alama za mipaka Pori Tengefu Loliondo umekamilika
●Vigingi 424 vyawekwa kama alama
●Barabara ya kilomita 108 yachongwa mpakani
●Kigingi Namba Moja maalum kumkumbuka askari aliyepoteza maisha.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo ametangaza kukamilika kwa zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika Pori Tengefu la Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha.
Majaliwa amepongeza washiriki wote wa zoezi hilo na kuwataka wananchi kuepuka taarifa hasi za upotoshwaji kuhusu eneo hilo kwani zoezi hilo limefanyika kwa nia njema ya kuhifadhi eneo hilo na kuwa hakuna wananchi wowote waliohamishwa.
“Eneo hili ni muhimu kwa kuwa na vyanzo vya maji na mazalia ya nyumbu ambayo ni muhimu kwa uwepo wa maeneo ya hifadhi za Serengeti na Ngorongoro”, amesema Majaliwa.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa wizara na taasisi zilizo chini yake wataendelea kusimamia maeneo yote ya uhifadhi kwa niaba ya wananchi.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amesema kuwa zoezi hilo limekamilika kwa wakati na kwa mafanikio makubwa. Ameongeza kuwa wameamua kumpa heshima askari Garlus Mwita aliyepoteza maisha akiwa katika zoezi hilo kwa kujenga mnara katika kigingi namba moja kama alama ya kumuenzi shujaa huyo.