
WaziriMkuu, Kassim Majaliwa amezitaka jumuiya za wafanyabiashara nchini kuendelea kuwa na imani na Rais Samia Suluhu Hassan kwani amedhamiria kutatua changamoto zinazohusu masuala ya kodi.
Amesema Rais Dkt. Samia anajali changamoto za wafanyabiashara na ndio maana ameunda timu mbalimbali kwa ajili ya kufanya mapitio ya kero za wafanyabiashara wafanye kazi zao kwa uhuru.
Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akijibu hoja zilizotolewa na Mwakilishi wa wafanyabiashara wa Halmashauri ya Makambako aliposimama na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo.
“Nataka niwatoe Mashaka Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan baada ya mapendekezo yenu wafanyabiashara yale kumi na tano, kufuatia mkutano na wafanyabiashara Kariakoo ameunda tume inayofanya mapitio ya mfumo wa kodi Tanzania na inaendelea kuzunguka nchi nzima kufanya kazi hiyo,” amesema.
Aidha, amempongeza Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato nchini sambamba na kuchukua hatua kwa watendaji wa Mamlaka hiyo ambao wanaenda kinyume na maadili yao ya kazi.
Pia, amemtaka kamishna huyo kuendelea kuboresha programu za utoaji wa elimu kwa mlipa kodi, ili kuondoa changamoto zinazowakabili wafanya biashara kuhusu masuala ya kodi.