
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ambaye pia ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025, huku akisisitiza kuwa wagombea wa chama hicho wataingia kwenye uchaguzi wakiwa na rekodi thabiti ya utekelezaji wa ilani ya chama.
Akihutubia wananchi katika Uwanja wa Nguzo Nane wilayani Maswa, mkoani Simiyu leo, amesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, CCM itaendelea kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana, ili wagombea wa chama wasiwe na kazi kubwa ya kueleza waliyoyafanya, bali waombe kura tu.
“CCM ni chama kikubwa, chama pendwa na chama kinachoaminiwa. Kina sera zinazotekelezeka, kikiahidi, kinatekeleza. Wanamaswa, leo mpo hapa na Mheshimiwa Nyongo (Mbunge wa Maswa Mashariki), anawapasha yanayotekelezwa ili mgombea wetu atakapofika hapa, kazi yake iwe ni ndogo ya kuomba kura,” amesema Majaliwa.
Amesema serikali kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za elimu, maji na afya ili kuboresha maisha ya wananchi.
“Chama cha Mapinduzi kwa uimara wake na sera yake, bado tutafanya kazi kwa nguvu zote, usiku na mchana ilimradi Watanzania mnaishi kwa amani na utulivu na huduma mnazipata kadiri mnavyozihitaji,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu amebainisha kuwa serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kila kijiji na kitongoji kinapata huduma ya maji safi na salama, kwa kuchimba visima na kuweka mitandao ya mabomba.