Majibu wa Rais Samia juu ya Moshi kuwa Jiji

0
58

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali inaendelea kupitia vigezo vinavyotakiwa kufuatwa ili kuufanya Mji wa Moshi kuwa Jiji kwani bado haijafikia.

Akizungumza na mamia ya wananchi waliokusanyika katika Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi, Rais Samia amesema kwamba, mbali na suala la vigezo, bado kuna suala la Vunjo kutaka kuwa halmashauri wakati umbali kutoka Moshi hadi Vunjo hauzidi kilomita 25.

Amesema serikali itaangalia vyote au kupanua halmashauri ya Moshi ili Vunjo nayo iwe sehemu yake.

“Lakini pia kuna suala la vigezo ambalo tukiangalia mji wa Moshi bado haujafikia, lakini niwaambie serikali tutalifanyia kazi. Tutaangalia uwezekano wa yote, kuvunja Vunjo iingia jijini au jinsi tutakavyoona inafaa kulingana na vigezo,” ameeleza.

Mchakato wa kufanya mji huo kuwa jiji umekuwa ukienda mbele na kurudi nyuma ambapo awali viongozi wa mkoa huo tayari walikuwa wamepitisha azimio la kuufanya mji huo kuwa Jiji.

Rais Samia leo ameendelea na ziara mkoani humo alimowasili jana, ambapo amezindua Barabara ya Sanya Juu – Elerai yenye urefu wa kilomita 32.2 ikiwa ni sehemu ya ujenzi/ukarabati wa barabara ya Bomang’ombe – Kamwaga yenye urefu wa kilomita 98.2.

Aidha, ameweka mawe ya msingi ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Mawezi na Daraja la Rau ambalo ujenzi wake unagharimu zaidi ya TZS milioni 900.

 

Send this to a friend