Majibu ya Polisi kuhusu madai ya ACT Wazalendo utata wa kifo cha diwani

0
37

Kufuatia tuhuma zilizotolewa na Chama cha ACT Wazalendo kupitia mitandao ya kijamii kuwa aliyekuwa diwani wa Kata ya Nyamgali, Majaliwa Abbas Hamis, kifo chake kina utata na kwamba hakikutokana na ajali, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limesema yeyote mwenye taarifa na ushahidi wa kweli tofauti na ambao umekusanywa aufikishe polisi.

Polisi wamesema taarifa zilizokusanywa hadi sasa kutokana na uchunguzi ni kwamba Januari 23, 2026 majira ya saa 4 usiku, zilipokelewa taarifa kuwa katika eneo la Kijiji cha Songambele kuna ajali ya mtu aliyekuwa anaendesha pikipiki.

“Askari polisi walifika katika eneo la tukio na kukuta kweli kuna mtu amegongwa na kufariki dunia na pikipiki ikiwa pale ikiwa imeharibika vibaya kutokana na kugongwa, na mahindi aliyokuwa amebeba yamemwagika na kusambaa barabarani,” imeeleza taarifa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa uchunguzi uliofanyika ulikuwa ni sambamba na kutumia simu aliyokutwa nayo marehemu ambayo ilisaidia kugundua kuwa aliyekuwa amegongwa na gari ambayo bado haijafahamika akiwa anaendesha pikipiki namba MC 709 BCW aina ya Kinglion iliyokutwa eneo la tukio ikiwa imeharibika vibaya ni Majaliwa.

“Uchunguzi bado unaendelea ili kubaini gari iliyomgonga na dereva aliyekuwa anaiendesha ni nani ili aweze kukamatwa kwa hatua nyingine za kisheria,” wamesema polisi.

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa baadhi ya watu kuacha tabia za kutengeneza taarifa za upotoshaji kwa lengo la kujenga chuki, hasira na kuzua taharuki kwa ndugu na wananchi wakati wa matukio kama hayo.

Send this to a friend