Majibu ya serikali kuhusu bima ya afya kwa wote

0
18

 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amesema kwamba kikosi kazi maalum kinafanyia maboresho pendekezo la kuwa na bima za afya wote, mpango ambao utatoa ahueni za matibabu kwa Watanzania wote.

Dkt. Gwajima amesema hayo akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua ni lini wimbo mzuri wa bima kwa wote utakamilika kwani umechukua miaka mingi sana, na bado haifahamiki mwisho ni lini.

“Suala hili ni kubwa, linahitaji kupita ngazi zote za maamuzi. Lianze kwenye wizara, liende kwa makatibu wakuu, liende kwenye baraza la mawaziri, liende kwenye kamati inayoshughulikia masuala ya sheria, ndio lifike bunge,” ameeleza Gwajima na kufafanua kwamba katika ngazi zote hizo, kuna maoni yanatolewa hivyo marekebisho yanafanyika.

Amesema suala hilo limeshatoka kwenye baraza la mawaziri na sasa linaboreshwa na baada ya hapo litapelekwa bungeni, na hivyo amewataka wananchi kuwa wavumilivu.

Ni miaka 9 sasa tangu mchakato wa bima ya afya kwa wote kuanza, mapango unaoaminiwa kuwa utaleta mapinduzi kwenye mfumo wa utoaji matibabu kwa wananchi.