Majukumu makubwa matatu yanayomsubiri Kinana

0
45

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana ambaye amechaguliwa na wajumbe wa chama hicho leo Aprili Mosi katika Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika jijini Dodoma amebainisha majukumu ambayo atayapa kipaumbele katika uongozi wake.

Kinana ambaye amepata kura 1,875 za wajumbe sawa na asilimia 100, amesema kuwa jukumu lake la kwanza ni kukiimarisha chama kiwe chama imara kinachokubalika na kuheshimika miongoni mwa watanzania.

Kinana ameahidi kuimarisha chama hicho kwa kusimamia demokrasia ndani ya chama kuwa imara, na kuongeza kuwa ili demokrasia iwe imara ni lazima wasimamie haki ya kuchagua na kuchaguliwa bila upandeleo wowote.

Jukumu lake la Pili ni kuhusiana na haki ya kutoa mawazo kwa wanachama. Amesisitiza kuwa ni lazima wanachama wawe huru kutoa mawazo yao, na kwamba ni lazima wawe tayari kumsikiliza kila mtu.

“Hakuna mwenye hakimiliki ya mawazo, Lazima tuwe tayari kumsikiliza kila mwanachama, tukiweza kuimarisha haki ndani ya CCM tutaimarisha haki nje ya CCM,” amesema Kinana.

Jukumu lingine ni kusimamia maelekezo, sera na ilani ya chama kwa kuikumbusha serikali, pia ameahidi kukomesha ukanda, ukabila na udini ndani ya Chama cha Mapinduzi.

Kinana amechukua nafasi hiyo kutoka kwa Philip Mangula ambaye ameng’atuka kwa hiari akiwa na miaka 81.

Send this to a friend