Mwaka 1991, wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) walianzisha Siku ya Mtoto wa Afrika (DAC) kama kumbukumbu ya uasi dhidi ya wanafunzi (16 Juni 1976) huko Soweto, Afrika Kusini.
Wakati huo, wanafunzi watoto wadogo waliandamana, mosi kupinga aina ya elimu duni ya kibaguzi waliyopea na serikali ya kibeberu, pili waliitaka serikali ya mzungu iwape ruksa kufundishwa kwa lugha zao wenyewe.
Siku ya Mtoto wa Afrika hutumika kuwakumbusha watoto hatua ya kijasiri waliyoichukua wenzao huko Afrika Kusini katika kulinda haki zao. Watoto wanakumbushwa kwamba wanaweza kuleta mabadiliko hata wakiwa wadogo.
Hivyo, Siku ya Mtoto inaadhimishwa kwa maslahi mapana ya watoto wa Afrika na inapaswa watu wazima kujitolea kwa hali na mali katika kushughulikia changamoto nyingi zinazokabili watoto katika bara zima.
Wazazi watambue kuwa familia ndio taasisi ya kwanza kuweka msingi wa maendeleo ya watoto kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa yaliyosainiwa na mataifa yaliyo mengi duniani, ikiwemo Tanzania.
Takwimu za kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto, zinaonesha watoto wamekuwa wakipitia magumu ikiwemo vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, utelekezwaji, vipigo, utumikishwaji wa kazi ngumu, mimba na ndoa za utotoni ambapo yote haya yanakatiza ndoto zao za kimakuzi na mendeleo.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hutumika pia kuwakumbusha viongozi, wananchi na vyombo vya habari kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kupiga hatua bila kutilia maanani mahitaji ya watoto, ikiwa ni pamoja na watoto masikini na walio na mazingira magumu zaidi kutengewa mafungu toka katika bajeti kuu ya serikali na zile za Halmashauri.
Kushindwa kuwekeza katika huduma muhimu na ulinzi wa watoto wote sio tu kunawanyima watoto haki zao lakini kutaingiza gharama kubwa zaidi baadaye kwa ajili ya maisha tegemezi watakayoishi, kunapoteza na kupunguza uzalishaji.
Chanzo: Sema Tanzania