
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla ameelekeza watia nia wa ubunge na udiwani waliolipishwa fedha za ziada wakati wa kuchukua fomu za ugombea wilayani Meatu mkoani Simiyu kurudishiwa fedha zao.
Hatua hiyo imetokana na malalamiko yaliyotolewa na mtia nia ya ubunge Jimbo la Meatu kupitia CCM, John Joseph G’wanambuke kueleza kutakiwa kulipa shilingi 500,000 ya ziada kwa ajili ya michango ya uendeshaji wa kampeni za uchaguzi mwezi Oktoba, mwaka huu.
“Mgombea anapaswa kutoa shilingi 500,000 ya kuchukulia fomu ya ubunge, na kwa udiwani shilingi 50,000. Hakuna fedha ya zaidi ya hapo. Kama kuna mgombea ametozwa fedha zaidi ya hicho kiasi kwa kisingizio cha michango ya kukiimarisha chama akachukue hela hiyo haraka sana […] Namwelekeza aende kwa Katibu wa Wilaya apewe hela yake,” amesema Makalla.
Makalla ameongeza kuwa kama kuna katibu wa chama ataendelea kudai kwamba fedha hiyo hairudishwi, basi atakuwa miongoni mwa makatibu ambao watachukuliwa hatua.







