Makamba: Mtanzania Joshua Mollel aliuawa na Hamas

0
63

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashiriki, January Makamba amesema Serikali ya Israel imeijulisha Tanzania kuwa Mtanzania Joshua Mollel aliuawa na kundi la Hamas mara tu baada ya kutekwa Oktoba 7 mwaka huu.

Waziri Makamba amesema amezungumza na baba mzazi wa Joshua kuhusu taarifa hiyo na Serikali inafanya taratibu za awali kuwapeleka Mzee Mollel na mwanafamilia mwingine nchini Israel ili kuzungumza na mamlaka ya nchi hiyo kwa ajili ya kupata taarifa zaidi kuhusu mpendwa wao.

“Kwa ridhaa ya familia, na itakapobidi, tutatoa taarifa za ziada katika siku zijazo,” amesema Waziri Makamba.

Joshua alitekwa pamoja na Clemence Mtenga ambaye naye aliuawa na mwili wake ulizikwa kijijini kwao Rombo mkoani Kilimanjaro Novemba 28 mwaka huu.