Makamba: Tutakutana Desemba kujipanga uharibifu mito

0
28

 

Waziri wa Nishati, January Makamba, ameeleza kwamba Wizara ya Nishati itaitisha mkutano maalum wa wadau wa matumizi na hifadhi ya rasilimali-maji katika mabonde na mito inayopeleka maji katika mabwawa na vituo vya kuzalisha umeme nchini ili kuweka mikakati madhubuti zaidi ya hifadhi na matumizi endelevu ya maji ya mito hiyo.

Waziri Makamba ameyasema hayo jana wakati alipotembelea Bwawa la Nyumba katika Bonde la Mto Pangani katika mwendelezo wa ziara yake ya kuzungumza na viongozi na wananchi kandokando ya mito inayoingiza maji kwenye mabwawa na vituo vya kuzalisha umeme. Waziri Makamba amesema kwamba Wizara na TANESCO ni wahanga sio tu wa ukame bali matumizi yasiyo endelevu ya maji. “Imefika wakati sasa sisi tusiwe tunayasubiri tu maji kwenye mabwawa na vituo vyetu vya kuzalisha umeme. Lazima na sisi tuwe na mkono katika kuhakikisha kuna usimamizi bora wa rasilimali hiyo ili ifike kwenye mabwawa yetu kwa kiwango cha kutosha kuzalisha umeme wa kutosheleza mahitaji, tusiwe tu walalamikaji wa uharibifu wa mito”, alisema Waziri Makamba. Aliendelea kueleza kwamba “tunatambua kwamba yapo mahitaji ya maji kwa ajili ya kilimo, kwa ajili ya mifugo, kwa ajili ya matumizi ya watu, kwa ajili ya uzalishaji umeme na kwa ajili ya ustawi wa ikolojia. Ni muhimu wadau wote tukakaa kwa pamoja na kutathmini hali halisi na kuimarisha utaratibu uliopo wa mgawanyo wa maji ili kila hitaji lipate maji bila kuathiri hitaji jingine”.

Waziri Makamba aliwataja wadau hao kuwa ni Wizara ya Maji, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ikijumuisha Wakuu wa Mikoa, Wilaya, na Wakurugenzi wa Halmashauri husika. Wadau wengine ni taasisi nyingine za Serikali zilizopo chini ya Wizara hizi, ikiwemo NEMC, Bodi za Mabonde ya Mito na Mamlaka za Maji, taasisi za utafiti na watumiaji wakubwa wa maji.

Waziri Makamba alisema “nafahamu kwamba hatuvumbui upya gurudumu, kuna kazi fulani imefanyika katika suala hili ila tunataka kuiboresha na kuiimarisha na kuhakikisha uratibu madhubuti na uwajibikaji wa pamoja katika kutekeleza tunayoamua kuyafanya. Kwahiyo tutaitisha mkutano huo mwezi ujao wa Disemba. Mkutano huo utatanguliwa na kazi ya watalaam ya kuchambua hali halisi, kupitia sheria na taratibu zilizopo, mapungufu yaliyopo, na mapendekezo ya hatua za kuchukua”.

Waziri Makamba alisema kwamba suala hili ni muhimu kwa Wizara anayoingoza kwasababu mbili “moja, wenzetu wanaohitaji maji ya kunywa au kumwagilia mazao au kulisha mifugo wana mbadala wa kupata maji kwa kuchimba visima. Sisi wazalishaji umeme hatuwezi kuzalisha umeme kwa maji ya visima. Tutaendelea kutegemea mtiririko wa uhakika wa mito. Sababu ya pili, tunao mradi mkubwa na wa gharama kubwa wa Mwalimu Nyerere Rufiji ambao utahitaji mtiririko wa uhakika wa maji, kwahiyo lazima tukae na tushirikiane na wenzetu kuhakikisha maji hayapotei kwa uharibifu wa mazingira”

Katika ziara yake kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu na kituo cha kuzalisha umeme katika bwawa hilo, Waziri Makamba ameshuhudia athari kubwa ya ukame na shughuli za uchepushaji mto kwa ajili ya shughuli za uvuvi katika vijiji vya Wilaya ya Simanjro, Mkoani Arusha. Bwawa la Nyumba ya Mungu huhifadhi maji na kuzalisha umeme wa Megawati 8 kisha maji hayo husafiri umbali wa kilomita 242 na kutegemewa kuzalisha tena umeme wa Megawati 21 katika kituo cha Hale na Megawati 68 katika kituo cha New Pangani Falls katika Wilaya ya Korogwe, Mkoani Tanga.

Hata hivyo, kutokana na ukame, uchepushaji mto na ukarabati wa mitambo katika kituo cha Hale, uzalishaji wa umeme katika vituo hivyo vitatu vya Bonde la Mto Pangani umeshuka kutoka uwezo wa Megawati 97 hadi Megawati 37 zinazozalishwa sasa. Kutokana na ukame mkali, zimebakia siku 44 tu, iwapo mvua hazitanyesha, kabla ya kulifunga kabisa Bwawa la Nyumba ya Mungu kutokana na kufikia kina cha chini kabisa ambapo uzalishaji umeme hauruhisiwi.

Send this to a friend