Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Tanzania Labour Party (TLP), Dominata Rwechungura amedai kujeruhiwa baada ya kushambuliwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Richard Lyimo akishirikiana na Naibu Katibu Mkuu, Yustino Rwamugila .
Tukio hilo limetokea siku ya Alhamisi Oktoba 24, katika Ofisi za Makao Makuu ya Chama hicho, Magomeni Usalama mkoani Dar es Salaam, baada ya kutokea kwa hali ya kutoelewana baina ya viongozi hao, ambapo imeelezwa kuwa Katibu huyo amekuwa akitumia mamlaka yake vibaya ikiwemo kuwafukuza watu uanachama pasipo sababu za msingi.
Akizungumza na Swahili Times, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Rwechungura amesema chama hicho kimekuwa na msuguano tangu mwaka 2023, baada ya kufariki kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, marehemu Augustino Mrema, ambapo Katibu Mkuu amekuwa akijichukulia maamuzi bila kushirikisha viongozi wengine pamoja na kuingilia majukumu yasiyomhusu.
“Juzi nilienda ofisini nikakuta kwenye ubao wa matangazo kuna majina 29 wote ni viongozi wa chama, kwamba hao watu wote wamefukuzwa pamoja na mimi, nikawauliza mnafukuzaje watu bila kuwapa taarifa? Na hicho ni kikao gani kwa sababu kikao cha kamati kuu, mimi Makamu Mwenyekiti ni kiongozi, hamkunitaarifu kwamba kuna kikao cha kamati kuu,” ameeleza.
Amesema alipofika ofisini siku inayofuata, kiongozi huyo alianza kumtolea maneno machafu huku akimfukuza ofisini hapo, na alipokataa kutii amri yake, alimnyanyua kwa nguvu akishirikiana Naibu Katibu wake “Nilianza kunyanyuliwa kwa nguvu ninapigwa mgongoni ninasukumizwa mpaka kwenye geti, nilipotoka pale nilikuwa na maumivu makubwa sana.”
Naye, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Eng. Aivan Maganza amesema si mara ya kwanza kiongozi huyo kufanya matukio ya namna hiyo, kwani amekuwa akiwatishia maisha watu zaidi ya mara mbili na wengine akiwatishia kuwafukuza uanachama pindi akihojiwa kuhusu mambo ya chama.
“Shida kubwa ni kwamba tulikuwa kwenye uchaguzi na yeye alishindwa kwenye uchaguzi wa Uenyekiti. Nyaraka za chama na mali zote anashikilia yeye toka Mrema amefariki, kikatiba nyaraka zinabidi zikae kwa Makamu Mwenyekiti au kama atabaki nazo yeye, basi atabaki nazo kwa maelekezo ya Makamu Mwenyekiti ila yeye hazioneshi, hatoi taarifa yoyote,” amesema.
Eng. Maganza amesema kwa sasa Katibu Mkuu na Naibu wake wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za shambulio la mwili huku Makamu Mwenyekiti akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Palestina.