Makonda aagiza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha achunguzwe kwa tuhuma za Rushwa

0
68

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha kuanza uchunguzi dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Eng. Juma Hamsini na baadhi ya wasaidizi wake kutokana na tuhuma za Rushwa na ubadhirifu wa fedha za walipa kodi zinazowakabili.

Akizungumza na wadau wa utalii mkoani humo leo, Makonda amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Missaile Mussa kuwasimamisha kazi watumishi wote waliotajwa kuhusika na tuhuma hizo ili kupisha uchunguzi.

Hatua hio imefuata baada ya Mwenyekiti wa waongoza watalii Mkoa wa Arusha, Wilbard Chambulo kudai kuwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wamekuwa wakitengeneza nyaraka bandia pamoja na kuchepusha baadhi ya makusanyo ya kodi zinazotokana na sekta ya Utalii.

Chambulo amemweleza Mkuu wa Mkoa kwamba watumishi hao wamekuwa na makampuni hewa ya utalii pamoja na kuwa na namba tofauti za ulipaji wa kodi na usajili hewa wa makampuni yenye kufanana na makampuni halisi ya utalii yalipo ndani ya Jiji la Arusha.

Aidha, Makonda amepiga marufuku kwa halmashauri zilizopo mkoani humo kutumia Polisi kwenda kudai kodi kwa wafanyabiashara na kuagiza zitumike teknolojia zaidi kwenye kukumbusha na kudai madai mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Arusha.

Send this to a friend