Makonda aanza kwa kutuma ujumbe kwa mawaziri na wakuu wa mikoa

0
42

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda ametoa angalizo kwa viongozi wakiwemo mawaziri wote, wakuu wa mikoa na watendaji wote kwamba chama hicho hakitosita kuwachukulia hatua endapo watabainika kuwa hawajafanya kazi zao kikamilifu.

Ameyasema hayo Oktoba 26, 2023 mkoani Dar es Salaam katika hafla ya mapokezi yake yaliyofanyika katika ofisi ndogo za chama hicho Lumumba mkoani Dar es Salaam ambapo amesema chama hicho ni sikio la Serikali na sauti ya wananchi, hivyo kazi yao ni kusikiliza kwa niaba ya serikali na kusema kero na matatizo ya wananchi kwa niaba yao.

“Sitakuwa tayari kuwa msemaji wa chama ambacho kimepewa dhamana na wananchi, na wanaomsaidia mheshimiwa mwenyekiti wanashindwa kutekeleza nisimame hadharani kusema uongo, hapana. Kila kiongozi wa serikali atabeba msalaba wake mwenyewe,” amesema.

Aidha, amewakosoa wanaotaka muungano wa Tanzania uvunjike ili wapate nafasi ya kuingia madarakani akituma salamu kwao kuwa vijana na watoto wote waliozaliwa ndani ya muungano hawako tayari kuwa historia ya wao kuuharibu muungano huo.

Tanzania yatenga hekta 20 Bandari Kavu ya Kwala kwaajili ya Zambia

Mbali na hayo, amesema chama hicho kupitia mwenyekiti Rais Samia Suluhu kimejitosheleza kwa hoja, hivyo anatoa salamu kwa jeshi la polisi kuruhusu vibali na ulinzi kwa vyama vya upinzani, huku akiiomba mamlaka ya anga kumpa kibali cha kuruka na helikopta Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kufanya ziara zake, kwa kuwa chama hicho hakitegemei kufanya figisu zozote kutokana na uwezo na utekelezaji wa ilani usio wa mashaka.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ofisi aliyekuwa Katibu NEC, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema ambaye ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais, Masuala ya Wanawake na Makundi Maalumu amemtaka Makonda kuendeleza chama hicho na kuhakikisha chama kinakwenda kushinda kwa kishindo chaguzi zake.

Send this to a friend