Makonda: Mapenzi ya Mungu ni makubwa kuliko mapenzi yangu

0
64

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amewashukuru wote waliomtumia salamu za pole baada ya kushindwa katika kura za maoni za kuwania kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kugombea ubunge katika Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Paul Makonda ameandika kuwa licha ya kilichotokea jana anaamini kuwa mapenzi ya Mungu yatatimia.

” Jambo moja kubwa na muhimu ni kuyajua mapenzi ya Mungu na katika hili, mapenzi ya Mungu ni makubwa kuliko mapenzi yangu,” ameandika mwanasiasa huyo kijana.

Aidha, amewashukuru wana Kigamboni kwa kumruhusu kuwa sehemu ya maisha yao.

Katika kura za maoni zilizopigwa jana Julai 20, 2020, Makonda alishika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia kura 122, akiwa nyuma ya Dkt. Faustine Ndugulile aliyepata jumla ya kura 190. Ndugulile ndiye alikuwa mbunge wa jimbo hilo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Watu mbalimbali walioandika maoni yao katika ujumbe huo wameonesha kumpa pole kiongozi huyo huku wakimtia moyo kwamba asikate tamaa.

Send this to a friend