Makosa manne yanayojirudia kila mara kwenye Bongo Movies

0
27

Kumekuwa na malalamiko mengi juu ya filamu za Kitanzania kuwa hazina uhalisia, huku watazamaji wakigeukia filamu za mataifa mengine hasa kwa kipindi hiki ambacho filamu nyingi na tamthilia kutoka nje ya nchi zinatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.

Gazeti la Nipashe linaandika juu ya makosa manne ambayo hufanyika mara kwa mara kwenye filamu za Kitanzania na kuchangia kuondoa uhalisia wa filamu hizo.

Kila mlinzi lazima awe ‘chale’
Ukiangalia filamu nyingi utagundua kuwa walinzi wa getini wanatumiwa wasanii wa vichekesho ambao lazima awe kama vile ‘zimemruka hivi’ huku nguo zao zikiwa kuu kuu.

Hii inaboa na kuzifanya sinema kuzoeleka na kutabirika. Kiuhalisia, jumba kubwa la mamilioni haliwezi kukabidhiwa kwa mtu wa namna hiyo alinde.

Tabia 6 za kila siku zinazosababisha uwe na kitambi

Jini lazima acheke, asubiri magari ili avuke
Waongozaji wa filamu wangepaswa wasubiri hakuna magari ndipo jini au mzimu avuke. Badala yake huanza kuangalia magari kabla ya kuvuka, hivyo kupoteza uhalisia.

Pia, mtu yeyote ambaye si wa kawaida kama jini au mzimu anapokutana na mtu ambaye anataka kumdhuru ni lazima acheke ‘hahahahahaha’. Huku ni kukariri kutoka kwenye filamu zilizopita, na si lazima itumike njia hiyo kila wakati.

Kutokubadili mwonekano
Inawezekana tatizo ni bajeti, lakini inapoteza sana uhalisia. Mhusika anakwenda Ulaya kwa muda mrefu, na wakati anaporudi uwanja wa ndege anaoneshwa akiwa na mtindo ule ule wa nywele na wengine hata kuwa na nguo ile ile. Kiuhalisia haikupaswa kuchukua picha mhusika anasafiri na kurejea siku hiyo hiyo, ilibidi akae hata wiki ili kubadilisha muonekano wake.

Jambazi lazima avae koti
Kwa hali ya kawaida mtu yeyote mwovu huficha uhalisia wake moyoni. Kwenye filamu za Kitanzania mtu yeyote mwovu hasa jambazi ni lazima avae koti refu jeusi na miwani meusi. Lengo si baya kuweka uhalisia, lakini si kila filamu mhusika anatakiwa ajulikane kuwa mtu mbaya kwa muonekano wake.

Send this to a friend