Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tanzania na Kenya kuhusu madereva wa malori

0
45

Kufuatia majadiliano yaliyofanyika kati ya maafisa wa Tanzania na Kenya, pande hizo mbili zimefikia makubaliano kuwa utaifa wa madereva watakaokutwa na maambukizi ya virusi vya corona hautawekwa wazi.

Taarifa ambayo imesainiwa na Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania na yule wa Kenya, Issack Kamwele na James Macharia, mtawalia, inaeleza kuwa taarifa hizo zitawasilishwa kwa mamlaka husika kupitia njia za kidiplomasia kwa ajili ya hatua zaidi.

“Watendaji wa malori watapimwa afya zao kabla ya kuanza safari kwa kuzingatia viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO), na watapatiwa vyeti vitakavyodumu kwa siku 14 kuonesha kuwa hawana maambukizi ya Covid-19. Kazi hiyo itafanywa na mamlaka itakayotambulika na pande zote mbili,” viongozi hao wamesema.

Kila gari (lori) litaruhusiwa kuwa na watu wasiozidi watatu, na kila nchi itaainisha maeneo ambapo madereva hao wataruhusiwa kusimama na kulala.

Nchi hizo pia zitawafanyia upimaji katika vituo maalum ambavyo vitatengwa kwa kazi hiyo.

“Endapo mtumishi wa lori ataonekana kuwa katika hatari kubwa ya maambukizi ya Covid-19, mmiliki wa lori ataruhusiwa kubadili watumishi hao na safari iendelee,” taarifa imeeleza.

Aidha, Wananchi wanaofanya shughuli za kilimo katika pande mbili za nchi hizo wataendelea na shughuli zao kwa sharti la kutambulika na mamlaka za serikali ikiwa ni pamoja na idara za uhamiaji na polisi.

Makubaliano hayo yamekuja ikiwa ni siku chache tangu sintofahamu zilipoibuka katika maeneo ya mipakani kutokana na madereva wa malori kuonekana kuwa chanzo kikubwa cha maambukizi ya corona kufuatia wengi wao kukutwa na maambukizi.

Send this to a friend