Makubaliano yaliyofikiwa na Tanzania na Uganda kuhusu madereva wa malori Mpaka wa Mutukula

0
46

Usafiri wa malori kati ya Tanzania na Uganda katika Mpaka wa Mutukula umerejea kufuatia nchi hizo mbili kufikia makubaliano juu ya hatua za kuchukua ili kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

Afisa Forodha katika mpaka huo upande wa Tanzania, William Mkenda amesema kuwa madereva wote watalazimika kupimwa maambukizi ya Covid-19 kwa kufuata vigezo vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo lakini bila kusitisha biashara mpakani hapo.

Mkenda amesema ulazima wa kuwapima madereva unalenga kuhakikisha kuwa hatari zote za kiafya zinazohusiana na virusi vya corona vinakabiliwa.

Ujumbe wa EAC uliofika mpakani hapo kujionea shughuli zinavyoendelea ulikutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya madereva ili kutambua changamoto zinazowakumba wakati wa kuvuka mpaka. Wakati wa majadiliano baadhi ya madereva walieleza kutoridhishwa na hatua zinazochukuliwa juu yao wakati wa utekelezaji wa hatua za kudhibiti corona.

Ujumbe huo umewatoa hofu madereva kwa kuwaeleza kuwa tayari maafisa wanaohusika na biashara na afya wa EAC wamekutana na kuweka vigezo vya namna madereva wanatakiwa kufanya wanapovuka mipaka wakati nchi wanachama zikitekeleza mikakati ya kudhibiti corona.

EAC imekuwa ikichukua hatua kadhaa kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona katika nchi wanachama ambazo ni pamoja na kugawa vifaa vya kupimia, mavazi maalum ya kujikinga (PPE), na maabara zinazotembea.

Send this to a friend