Malanga alivyokuwa nyuma jaribio la mapinduzi DRC na jinsi Marekani inavyohusishwa

0
43

Jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Felix Tshisekedi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) limeleta taharuki na wasiwasi kuhusu usalama na utulivu wa kisiasa katika nchi hiyo yenye changamoto nyingi.

Tukio hilo lililoshuhudiwa alfajiri ya Jumapili linaloaminiwa kuongozwa na Christian Malanga, mwanasiasa na aliyekuwa afisa wa jeshi wa zamani ambaye alionekana kuwa mhusika mkuu wa shambulio hilo. Shambulio hilo lililenga makazi ya mshirika wa karibu wa Tshisekedi, Kamerhe na hata Ikulu ya Rais, japokuwa hakuwepo katika makazi hayo.

Christian Malanga Musumari, alikuwa mfanyabiashara tajiri, mwanasiasa, na aliwahi kuwa nahodha wa jeshi la Congo. Alikuwa mkazi wa Marekani ambapo familia yake ilipata hifadhi alipokuwa mdogo.

Ingawa Malanga aligombea uchaguzi wa ubunge mwaka 2011, alikamatwa na kuzuiliwa kwa wiki kadhaa chini ya uongozi wa Rais wa zamani, Joseph Kabila. Baada ya kuachiliwa, Malanga alienda Marekani ambapo aliunda chama cha upinzani cha United Congolese Party (UCP).

Sababu za aliyekuwa Waziri nchini Gambia kuhukumiwa miaka 20 jela

Kwa miaka mingi, Malanga alifanya kampeni ya uhuru wa kidini barani Afrika na akaongoza mipango ya mafunzo ya kupinga ufisadi kwa vijana wa Kiafrika barani Ulaya.

Maafisa walisema Malanga alijaribu kufanya jaribio la mapinduzi mwaka 2017 japokuwa hawakutoa maelezo zaidi.

Katika video iliyorushwa moja kwa moja kwenye mtandao wa Facebook wakati wa shambulio la Jumapili, Malanga alimtishia Rais Tshisekedi na kuimba “New Zaire!” [hapo awali DRC iliitwa Zaire], “Sisi, wanamgambo, tumechoka, “Hatuwezi kuendelea na Tshisekedi na Kamerhe, wamefanya mambo mengi ya kijinga katika nchi hii”.

Picha zilizotolewa baadaye kwenye mitandao ya kijamii zilionesha mwili wa Malanga na wapiganaji wengine ambapo maafisa walisema aliuawa baada ya kukataa kijisalimisha na kurushiana risasi huku wengine takribani 50 wakikamatwa wakiwemo raia watatu wa Marekani.

Mojawapo ya maswali yanayozua utata ni ikiwa kulikuwa na ushiriki wa Wamarekani katika jaribio hili la mapinduzi. Kulingana na taarifa, watu watatu waliokamatwa baada ya shambulio walikuwa raia wa Marekani, ikiwa ni pamoja na mtoto wa Malanga, Marcel (21). Hata hivyo, madai hayo hayajathibitishwa na bado na uchunguzi unaendelea kuhusu uhusika wao.

Lucy Tamlyn, Balozi wa Marekani nchini DRC ameeleza kuwa Marekani itashirikiana na mamlaka za DRC kikamilifu katika uchunguzi wa vitendo hivyo vya uhalifu na kuwawajibisha raia wa Marekani yeyote aliyejihusisha na vitendo vya uhalifu.

Tshisekedi bado hajatoa maoni hadharani na hasa jinsi maswali yanavyoendelea kuibuka juu ya jinsi wapiganaji wa Malanga walivyofanikiwa kuvunja usalama wa makazi ya Rais.