Malawi: Wakazi walazimika kupika viazi vyenye sumu ili kustahimili njaa

0
15

Wakazi waishio vijijni nchini Malawi wanalazimika kuchimba viazi vya porini ambavyo vina hatari ya kuwa na sumu ili kupata chakula baada ya mazao yao kuteketea shambani kutokana na ukame ulioikumba nchi hiyo.

Wakazi hao wamesema watu hufariki au kuugua kutokana na kula viazi hivyo, na sasa inawalazimu kuichemsha kwa muda mrefu huku kila wakati wakibadilisha maji ya kupikia ili kuondoa sumu.

“Hali yetu ni mbaya sana, tunakufa njaa,” amesema bibi mwenye umri wa miaka 76, Manesi Levison, alipokuwa akiangalia sufuria ya viazi vya porini vyenye ladha chungu, ambavyo vinapaswa kupikwa kwa saa nane ili kuondoa sumu.

Malawi ni moja ya nchi maskini zaidi duniani, na idadi kubwa ya wananchi wake wanategemea kilimo kinachotegemea mvua.

Ukame wa mwaka huu uliosababishwa na El Nino, unaathiri asilimia 44 ya maeneo ya kilimo nchini Malawi na hadi asilimia 40 ya watu wake, ambao ni takriban milioni 20.4, kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (WFP).