Rais wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera aliwasili nchinj Tanzania Jumatano Oktoba 7 mwaka huu kwa ajili ya ziara ya kitaifa ya siku tatu (hadi tarehe 9), lakini alikatisha ziara hiyo na kurejea nchini mwake mapema.
Dkt. Chakwera alitarajiwa kuondoka nchini Tanzania leo, lakini aliondoka Tanzania jana jioni (Oktoba 8, 2020), akipunguza siku moja katika ziara yake.
Ikulu ya Malawi imesema kuwa kiongozi huyo alikatisha ziara yake na kurejea nchinj humo kwani alitakiwa kushughulika mambo kadhaa ya haraka ya ndani ya nchi.
Kiongozi huyo anatarajiwa kuhudhuria maandamano yaliyoandaliwa na wanawake kupinga kukosekana kwa usawa wa kijinsia yanayofanyika leo.
Wanawake hao wanaandamana kufuatia Rais Chakwera kushindwa kutimiza takwa la kuhakikisha uteuzi wa wake katika ofisi za umma unazingatia usawa wa kijinsia wa 60:40.
Rais Chakwera katika hotuba yake ya Jumatatu ya kuadhimisha siku 100 madarakani alisema anahitaji muda zaidi kufanikisha takwa hilo.
Akiwa nchini Tanzania Dkt. Chakwera alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Dkt. Magufuli kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, lakini pia alikutana na wafanyabiashara na alishiriki hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye stendi mpya ya kimataifa ya mabasi ya mikoani na nje ya nchi jijini Dar es Salaam.
Dkt. Chakwera mbali na kuwa Rais wa Malawi, lakini pia ni waziri wa ulinzi wa nchi hiyo.