Malema: Hakuna atakayemkamata Putin akiwasili Afrika Kusini

0
38

Chama cha upinzani cha Afrika Kusini, Economic Freedom Fighters (EFF), kimesema Rais wa Urusi, Vladimir Putin anakaribishwa kuzuru Pretoria licha ya hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ambayo Afrika Kusini ni mwanachama.

Kiongozi wa EFF, Julius Malema amesema hakuna mtu atakayemkamata Rais huyo akiwa Afrika Kusini kwa kuwa nchi ya Urusi ina mchango mkubwa katika kuunga mkono mapambano ya uhuru.

“Putin anakaribishwa hapa, hakuna atakayemkamata Putin. Ikibidi tutaenda kumchukua Putin kutoka uwanja wa ndege hadi kwenye mikutano yake. Atahutubia, atamaliza mikutano yake yote, na tutamrudisha uwanja wa ndege.

Tunawajua marafiki zetu, tunawajua watu waliotukomboa, tunawajua watu waliotuunga mkono,” amesema.

Rais mteule wa Nigeria aenda mapumziko Ulaya

Rais Putin anatarajia kwenda Afrika Kusini na kushiriki mkutano wa kilele wa Brics (Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini) mwezi Agosti mwaka huu.

Mahakama ya ICC, ambayo Afrika Kusini imetia saini, imemshutumu Putin kwa uhalifu wa kivita ambao ni pamoja na utekaji nyara wa watoto wa Ukraine katika uvamizi unaoendelea nchini Ukraine.

Afrika Kusini ina uhusiano wa karibu wa kidiplomasia na Moscow licha ya kupingwa na nchi za Magharibi. Mwezi uliopita, jeshi lake la wanamaji lilifanya mazoezi ya pamoja na vikosi vya Urusi katika pwani ya Afrika Kusini.

Send this to a friend