Mali za mtoto wa Rais zauzwa kununua chanjo ya UVIKO19

0
35
Wizara ya Sheria ya Marekani imesema kuwa fedha zilizopatikana kwa kuuza mali za Teodoro Nguema Obiang Mangue, Makamu wa Rais wa Equatorial Guinea zitatumika kununua chanjo kwa ajili ya taifa hilo la Afrika.
 
Marekani imesema kuwa mali hizo za Obiang ambaye ni mtoto wa Rais wa nchi hiyo, Teodoro Obiang Nguema Masongo, zilipatikana kwa njia zisizo za halali.
 
Wizara hiyo imesema kuwa TZS bilioni 44 kati ya TZS bilioni 59 zilizopatikana zitapelekwa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kununua chanjo za kupambana na maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19).
 
Aidha, TZS bilioni 14.4 zitatumika kununua vifaa na vifaa tiba na kisha vitapelekwa nchini Equatorial Guinea kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.
 
Taarifa ya Marekani imeeleza kuwa mwaka 2011 akiwa Waziri wa Kilimo, kiongozi huyo alichota zaidi ya bilioni 692. Pia mwaka 2014 alitakiwa kuuza jumba lake la kifahari lililopo Carlifonia kwa TZS bilioni 69.2.
Send this to a friend