Mama adaiwa kumteka mtoto wake ili mume atoe milioni 20

0
44

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limesema linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kumteka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitano, mwanafunzi wa shule ya Awali ya Isaiah Samartan jijini humo ambaye aliripotiwa kupotea Mei 15, mwaka huu.

Akitoa taarifa hiyo Msemaji wa Jeshi la Polisi Naibu Kamishna wa Polisi, David Misime amesema tukio hilo liliripotiwa na baba mzazi wa mtoto Layson Mkongwi, mfakanyakazi wa Kampuni binafsi ambaye alipokea simu kutoka kwa mtu asiyefahamika na kumweleza kuwa hatampata mtoto wake hadi atakapomtumia kiasi cha shilingi milioni 20.

Ameongeza kuwa baada ya kupokea taarifa hizo Jeshi lilianza uchunguzi na kufanikiwa kumpata mtoto akiwa salama pamoja na mtuhumiwa, Winfred Martin Komba (36) mkazi wa Vingunguti Dar es Salaam ambaye ndiye aliyekuwa akimpigia simu baba mzazi wa mtoto na kumtishia atoe fedha.

Watuhumiwa wengine waliokamatwa ni mama mzazi wa huyo mtoto, Agnes Jacob Mwalubuli mkazi wa Isyesye Mbeya ambaye alipanga njama na mtuhumiwa ili kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa baba mzazi wa mtoto huyo.

Mtuhumiwa Wilfred Komba baada ya kuhojiwa alieleza kuwa baada kupanga njama hizo alifanikiwa kumchukua mtoto huyo na kwenda kumficha kwa rafiki yake aitwaye Hamida Gaudence anayeishi Mbeya ambako ndiko mtoto alikopatikana.

Misime amesema tukio hilo limechukuwa muda mrefu kutokana na kila jambo ambalo Polisi walikuwa wanapanga kwa kumshirikisha mama mzazi wa mtoto huyo wakidhani ana uchungu na mtoto wake lakini yeye alikuwa akimfikishia taarifa mtuhumiwa mwenzake hivyo kumfanya aendelee kujificha.

Aidha, amesema Jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa hao kwa ajili ya kukamilisha taratibu nyingine ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.