Mama amuuza binti yake kwa mganga wa kienyeji
Mahakama nchini Afrika Kusini imemkuta na hatia mama aitwaye Racquel “Kelly” Smith na watu wengine wawili ya kumsafirisha na kumteka nyara binti yake mwenye umri wa miaka sita, Joshlin Smith, ambaye hajulikani alipo tangu Februari 2024.
Katika kesi hiyo iliyochukua miezi miwili, mashahidi mbalimbali walitoa ushahidi kuwa Racquel “Kelly” Smith, mwenye umri wa miaka 35, alikiri kwao kuwa alimuuza binti yake Joshlin Smith mwezi Februari 2024 kwa randi 20,000 [TZS takriban milioni 3].
Jaji wa mahakama amesema ushahidi wa mashahidi 35 wa upande wa mashtaka ulimwaminisha kuwa Smith pamoja na mpenzi wake na rafiki yao wa karibu walikuwa na hatia ya usafirishaji haramu wa binadamu na utekaji nyara.
Awali, Smith alipata huruma kubwa kutoka kwa umma baada ya kuripoti kupotea kwa Joshlin mwezi Februari 2024, lakini baadaye ushahidi kutoka kwa mwalimu wa mtoto, mchungaji, na majirani ulieleza kuwa mama huyo alikuwa ameonesha dalili za kutokuwa na wasiwasi katika kipindi chote cha utafutaji wa mtoto wake.
Mashitaka yameeleza kuwa Smith alimuuza Joshlin kwa mganga wa kienyeji aliyedaiwa kuvutiwa na macho ya mtoto huyo na ngozi yake yenye weupe.
Mama huyo sasa anakabiliwa na hukumu kali ambayo inaweza kuwa hadi kifungo cha maisha.