Mara zote mwanamke akiwa hataki kubeba mimba, hutumia njia mbalimbali kuhakikisha hilo linafanikiwa. Vivyo hivyo, ukitaka kubeba ujauzito, kuna mambo ya kuzingatia, kuhakikisha unajifungua mtoto mwenye afya njema.
Ama ni mara yako ya kwanza au ya sita, bado kuna mambo ya msingi unayotakiwa kuzingatia. Siku zote epuka kufanya kitu kwa mazoea hata kama ndicho unachokifanya kila siku.
Fanya mambo haya kuuandaa mwili wako kubeba ujauzito na kujifungua mtoto mwenye afya:
Weka mipango
Hakikisha kupata ujauzito hakutokei kama ajali. Weka mpango kwamba kipindi fulani nitabeba ujauzito, jiandae kisaikolojia, ili kuuandaa mwili kupokea ugeni huo.
Ushauri wa Daktari
Kabla ya kupata ujauzito ni vyema ukaonana na mtaalamu wa afya kuhusu mambo ya kufanya kabla ya ujauzito. Madaktari hushauri mama anayetaka kubabeba mimba kuanza kutumia vidonge vya folic acid miezi kadhaa kabla, hivyo ni vyema ukaenda kituo cha afya ili ujue nini cha kutumia au cha kuacha (dawa, chanjo, staili za maisha).
Meza Folic Acid
Vidonge hivi ni vya vitamin B. Mwanamke anashauriwa walau kumeza vidonge hivi si chini ya mwezi mmoja kabla ya kupata ujauzito ili kuzuia mtoto kupata matatizo ya ubongo na uti wa mgongo na mengine.
Epuka pombe, sigara na baadhi ya dawa
Kuvuta sigara, unywaji pombe na baadhi ya dawa vinaweza kusababisha matatizo kwa mjamzito na mtoto kama kujifungua mtoto njiti, changamoto za kujifungua na kufariki kwa mtoto.
Mazingira hatarishi
Epuka kukaa kwenye mazingira yenye kukuweka kwenye kemikali kali kama systhetic chemicals, vyuma, mbolea kwani zinaweza kuathiri mfumo wa uzazi.
Uzito wa mwili
Watu wenye uzito uliopitiliza wapo kwenye hatari kubwa ikiwemo wa changamoto wakati wa kujifungua, magonjwa ya moyo, kisukari na saratani. Aidha, wenye uzito chini ya kiwango pia wapo kwenye hatari ya kupata matatizo ya afya. Njia bora ya kuwa na kiwango sahihi cha uzito ni mtindo mzuri wa maisha, kula kwa kiasi, mazoezi na kupata muda wa kutosha kulala.
Ugomvi
Ugomvi unaweza kukusababishia athari za kimwili ikwemo mfumo wa uzazi hivyo ni vyema ukaepuka hatari zozote zinazoweza kusababisha ugomvi.
Historia ya familia
Kufahamu historia ya familia yako ni muhimu kwa afya ya mwanao, kwani utaweza kujua kama kuna mtu mwenye tatizo kama seli mundu, tatizo la moyo. Unapojua haya matatizo mapema, utaweza kuchukua tahadhari na kupeuka mtoto kufariki au changamoto nyinginezo.
Afya ya akili
Unahitaji kutokuwa na msongo wa mawazo au matatizo mengi ya afya ya akili kabla na wakati wa ujauzito. Hali kama wasiwasi, chuki, mashaka hazishauriwi, hivyo unapoona hali imezidi, pata ushauri wa wataalamu.
Ujauzito wenye afya
Mara unapopata ujauzito, hakikisha unaulea na unakuwa wenye afya njema. Hudhuria kliniki mara kwa mara, na kunapotokea changamoto yoyote, pata ushauri wa kitabibu.