Mambo 16 makubwa aliyosema Rais Samia akihojiwa na Azam TV
1. Kilichomshtua zaidi haikuwa kukabidhiwa jukumu la kuiongoza Taifa, bali sababu iliyopelekea kukaabidhiwa dhamana hiyo ambayo ni kifo cha Rais Dkt. John Magufuli kilichowashtua hata Watanzania.
2. Miradi yote ya kimkakati iliyoanzishwa katika awamu ya tano (JNHPP, SGR, Madaraja) ina tija kubwa katika wimbi la nne la mapinduzi ya viwanda.
3. Wanaosema kuwa Rais anasafiri sana wafanye tathmini ya safari zake kwani katika maeneo mengi aliyokwenda kama Kenya, Uganda, Dubai, Umoja wa Ulaya, Marekani amerejea na fursa za kibiashara, kitalii na uwekezaji.
4. Royal Tour maana yake ni kuipeleka Tanzania ulimwenguni. TZS bilioni 7 zilizotumika kuandaa filamu hiyo zimetolewa na wafanyabiashara na kuwa ni ndogo ikilinganishwa na manufaa ambayo yameanza kupatikana.
5. Huwezi kuchukua jambo kwa kusikia tu. Wanaosema vitendo vya rushwa na dawa za kulevya vimerudi watoe takwimu kwa sababu ripoti za kimataifa zinaonesha kwamba hali ya rushwa Tanzania iko chini.
6. Tanzania inakusidia kutia saini mkataba wa kuchakata gesi asilia (LNG) mkoani Lindi ambayo itauzwa hata nje ya Afrika. Aidha, inaendelea kutekeleza miradi mingine ya kuzalisha umeme kama upepo, jua, maji, jotoardhi, ili kumaliza tatizo la umeme na kufanya ukarabati wa mitambo ili kuwa na umeme wa uhakika.
7. Tanzania bado iko uchumi wa kati, lakini ukuaji uchumi wa ndani ndio umeshuka kutoka asilimia 6.8 hadi asilimia 4 kutokana na athari za UVIKO19. Mategemeo ni kuwa mwaka 2025 ukuaji wa uchumi utarudi katika asilimia 6.8 au zaidi.
8. Kuhusu madai ya ugumu wa maisha, Kusini mwa Afrika hali ya maisha ya Watanzania nzuri kuliko nchi nyingine, watu wanalalamika bei ya mafuta, Marekani mafuta ni ghali kuliko Tanzania.
9. Serikali inakwenda kufuta kodi iliyowekwa kwenye mafuta ghafi ya kula yanayoingizwa nchini, ili yachakatwe na kuwezesha upatikanaji wa mafuta ya kula ya kutosha. Amesema sababu za mafuta kupanda ni kuathirika kwa kilimo cha alizeti na kodi hiyo.
10. Amesema ukitangaza kupandisha mshahara na bidhaa zinapanda. Mwaka 2021 japo hakutangaza kupandisha mishahara, hatua mbalimbali zilichukuliwa kuboresha maslahi yao ikiwa pamoja na kufuta naa kupunguza kodi na mikopo, na hivyo kuwanufaisha watumishi kuliko hata wangepandisha mishahara.
11. Baadhi ya wakaguzi wa ndani hawafanyi kazi ndio maana kasoro zinaibuliwa katika ripoti ya Mdhabiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Amesema huwa wanachukua hatua kwenye hoja hizo lakini kwa vile hawajibii kwenye kamera, wananchi wanadhani hatua hazijachukuliwa.
12. Deni la Taifa bado ni himulivu, lakini limekuwa kwa sababu ya mikopo ya ujenzi wa miundombinu na miradi kama Bwawa la Nyerere, SGR, madaraja. Pia Tanzania imetoka kwenye ngazi ya chini kwenda kwenye ngazi ya kati ya hatari ya mikopo.
13. Tatizo la ajira ni dunia nzima, lakini jitihada zake anaposafiri nje ni kuvutia wawekezaji ili kuzalisha ajira, kujenga vyuo vya ufundi kila wilaya ili wanufaike, kujenga chuo cha TEHAMA Dodoma, na kutumia taasisi kama COSTECH, SIDO kukuza vijana wengi, pamoja ma kuboresha mfumo wa elimu iwe zaidi elimu ujuzi.
14. Kwenye muungano, ndoto yake ni kuona unakuwa imara zaidi.
15. Amesema kuwa hakatai uwepo wa katiba mpya, lakini ni wakati wa kuzungumza hayo. Amesema anasubiri kamati ya vyama vya siasa kuona italeta mapendekezo ya namna gani.
16. Maoni ya wadau yanaendelea kukusanywa ili kuona nini cha kufanya katika Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inayoruhusu mtoto wa miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi. Aidha, amesema maboresho ya elimu na sera ya elimu bure vitapunguza ndoa za utotoni.