Mwanamke anapofikisha miaka 40, ni muhimu kuzingatia afya ya mwili, afya ya akili, na afya ya uzazi kwani umri huo na kuendelea unamweka katika hatari ya kupata matatizo mbalimbali ikiwa hatafuata kanuni na taratibu za kiafya.
Haya ni mambo kadhaa ya kuzingatia ili kujikinga na magonjwa na kuishi umri mrefu;
Zingatia mazoezi mepesi
Fanya mazoezi mepesi na kazi za nyumbani zinazoushughulisha mwili wako kama usafi wa mazingira na kazi za bustani. Kwa siku angalau fanya mazoezi ya kutembea kwa dakika 30 hadi 60 au tembea kilomita mbili katika siku tano za wiki.
Epuka ulaji holela
Unapaswa kuepuka ulaji holela wa vyakula ikiwemo chumvi nyingi, sukari nyingi, vyakula vya wanga na mafuta mengi na badala yake unashauriwa kula zaidi mbogamboga na matunda pamoja na kunywa maji mengi angalau glasi 10 kwa siku.
Pumzika
Ni muhimu ikiwa utapata muda wa kutosha wa kulala na kupumzika katika maeneo rafiki yasiyo na usumbufu. Kiafya unashauriwa kulala saa sita hadi nane kwa siku.
Fanya uchunguzi wa kiafya
Ni muhimu kujitokeza kufanya uchunguzi wa matatizo ya afya yanayomgusa mwanamke moja kwa moja ikiwemo saratani ya mlango wa uzazi na matiti, pia fanya uchunguzi wa jumla angalau mara moja kwa miezi sita.
Epuka matibabu yasiyo rasmi
Ni kawaida kwa baadhi ya wanawake kushawishika na baadhi ya matibabu wanayokutana nayo mitandaoni au mitaani kama vile dawa za kupunguza unene na virutubisho ambavyo wakati mwingine hutolewa na watu wasio na ujuzi wa mambo ya tiba, hivyo ni vyema kuepuka tiba hizo ambazo si rasmi kwaajili ya afya yako.
Uchunguzi: Wanawake watumia vidonge 12 vya Flagyl kuzuia mimba
Hakikisha una bima ya afya
Ni muhimu kuwa na bima ili kukusaidia wakati wa uchunguzi wa mara kwa mara wa afya yako.
Chanzo: Mwananchi