
Ni kawaida kwa wengi kutamani kurudisha mahusiano baada ya kuachana na watu waliowapenda sana. Hata hivyo, jitihada za kurudisha penzi zinaweza kuwa na matokeo tofauti kulingana na njia unazotumia.
Kuna mambo ambayo ukifanya, si tu kuwa unaweza kumkimbiza mpenzi wako zaidi, bali pia unaweza kujidhalilisha na kupoteza heshima yako. Haya ni baadhi ya mambo ya kuepuka:
1. Kujidhalilisha kupita kiasi
Kupiga magoti hadharani, kulia mara kwa mara au kuomba msamaha kila saa kunaweza kuonekana kama kutokuwa na thamani binafsi. Kujidhalilisha hakumvutii mtu, bali kunamchochea kukudharau zaidi.
2. Kumfuatilia kila mahali
Kumuandama kila anakokwenda, kumchunguza kupitia marafiki au mitandao ya kijamii ni tabia inayochosha na inaweza kuonekana kama usumbufu. Badala ya kumfanya akukumbuke kwa mema, anaweza kuona kama unamuandama au kumvizia.
3. Kutumia huruma kama njia ya kumrudisha
Wengine hutumia magonjwa ya kughushi, matatizo ya kifamilia au hali za huzuni ili wapate huruma. Upendo wa huruma si wa kweli, na mara nyingi unadumu kwa muda mfupi tu. Kama mtu anapaswa kurudi, na arudi kwa sababu anakupenda kweli.
4. Kumlaumu au kumbebesha makosa yote
Kama mna nafasi ya kuzungumza, usitumie nafasi hiyo kumkosoa tu au kumweleza ni jinsi gani alikuwa mbaya. Mahusiano huvunjika kwa sababu mbalimbali, na mara nyingi kila mmoja anakuwa na mchango wake. La muhimu ni kuelewa makosa na kujifunza kutoka nayo.
5. Kulazimisha arudi bila ridhaa
Usilazimishe mtu arudi kwenye mahusiano wakati hajawa tayari au hataki. Penzi la kulazimishwa halina furaha, na litawachosha wote wawili. Mpe muda na nafasi ya kufikiria. Kama ni wako, atarudi kwa hiari.
6. Kujilinganisha na mpenzi mpya
Kujilinganisha na mtu mwingine, au kumchafua mpenzi wake mpya si suluhisho. Hii huonyesha wivu na kukosa kujiamini. Onesha thamani yako bila kushusha wengine.
7. Kutangaza matatizo yako mitandaoni
Kuweka matatizo yako ya kimapenzi mitandaoni, kulalamika kila sehemu au kueneza habari kwa watu wa karibu ni njia nyingine ya kujidhalilisha. Unaposhindwa kuwa mtulivu, unaonesha kuwa hukujifunza kutokana na yaliyopita.