Mambo 7 ambayo Tundu Lissu amemueleza Rais Samia

0
32

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu ameitikia ombi la Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu la kukutana nae, ambapo wamekutana Brussels nchini Ubelgiji.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, wawili hao wamezungumza masuala ya ustawi wa Tanzania.

Hata hivyo, kupitia ukurasa wake wa Twitter, Lissu ameweka wazi mambo aliyosema kwamba ndio wamezungumza na Rais Samia, mazungumzo ambayo yameibua hisia chanya.

Lissu ametaja mambo aliyowasilisha kwa Rais kuwa ni, kwanza, kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA na wenzake watatu ifutwe na waachiwe bila masharti kwani haikinufaishi chama tawala, CCM, wala CHADEMA.

Pili, amewasilisha suala la mikutano ya vyama vya siasa kwamba iruhusiwe na vyama hivyo vipewe ulinzi na polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Tatu, suala la Katiba mpya ambapo amemsihi Rais Samia kwamba hiyo ni alama na kumbukumbu kubwa anayoweza kuwaachia Watanzania.

Nne, ni suala la Watanzania waishio uhamishoni, kwamba Rais atamke kwamba wanakaribishwa nchini na watakuwa salama ili waweze kuridi.

Tano, ametaka wale wote waliohusika katika shambulio dhidi yake mwaka 2017 wawajibishwe kwa mujibu wa sheria. Pia amezungumza suala la kuvuliwa ubunge na kunyimwa stahiki zake, akieleza kwamba hayo yamefanyika kinyume na sheria.

Sita, ni suala la Wabunge 19 wa Viti Maalum ambao amesema kwamba hawako bungeni kihalali kwani tayari walishavuliwa uanachama wao. Lissu amesema suala la rufaa sio tiketi ya kuwaacha bungeni, na kwamba kuendelea kuwalipa fedha ni kuliibia Taifa.

Jambo la saba, Lissu amesema amemuomba Rais kuponya majeraha katika nchi, na hilo lianze kwa kutimiza ahadi yake ya kukutana na vyama vya upinzani.

Lissu amesema Rais Samia amemueleza kuwa ameyapokea na kwamba atayafanyia kazi.

Rais Samia yupo Ubelgiji akiendelea na ziara ya kikazi aliyoianza mara baada ya kumaliza ziara yake nchini Ufaransa.

Send this to a friend