Mambo matano yatakayojadiliwa kwenye mkutano anaohudhuria Rais Samia, Senegal
Rais Samia Suluhu Hassan leo Julai 6 ameondoka nchini kuelekea Dakar, nchini Senegal kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa (IDA Summit for Africa).
Viongozi wa nchi wanachama 39 kutoka Afrika wanatarajiwa kuhudhuria Mkutano huo Julai 7, mwaka huu utakaoongozwa na Rais wa Senegal, Macky Sall.
Mkutano huo kwa ujumla unalenga kuzikwamua nchi za Afrika kutoka kwenye mdodoro wa uchumi ambao umechangiwa na janga la UVIKO19, mabadiliko ya tabia ya nchi, njaa, na vita vya Urusi na Ukraine. Lengo la mkutano huo ni kujenga uchumi himilivu utakaoiwezesha Afrika kuendelea na mabadiliko ya kiuchumi.
Majadiliano katika mkutano huo, utaangazia zaidi katika maeneo makuu matano:
1. Mabadiliko ya kiuchumi;
2. Kilimo, ufugaji na usalama wa chakula;
3. Rasilimali watu;
4. Ubunifu wa kidigitali na kiteknolojia pamoja na
5. Nishati mbadala.
IDA ni mojawapo ya vyanzo vikubwa zaidi vya fedha kwa ajili ya kupambana na umaskini uliokithiri katika nchi zenye kipato cha chini zaidi duniani. Afrika ni mnufaika mkubwa zaidi wa IDA ikiwa na nchi 39, na imepiga hatua kubwa katika kuboresha rasilimali za maendeleo katika miongo sita ya ushirikiano na Benki ya Dunia.