Mambo saba yanayosababisha wahitimu wa vyuo kuwa masikini

0
43

Wanafunzi wengi wanapohitimu masomo yao hutegemea na huamini pia kuwa vyeti vyao ndivyo vitakavyowakomboa. Lakini ni ukweli mchungu kwamba hiyo si kweli, badala ya kukazana kutembea na vyeti, weka juhudi katika kutumia fursa zinazojitokeza mbele yako.

Endapo mtu akikupa nafasi ya kufanya kitu, na huna uhakika kama utaweza kukifanya, kubali kukifanya, kisha jifunze namna ya kukifanya. Wenye uwezo wa kukariri ndio wanaofanikiwa shuleni, lakini katika maisha wenye ubunifu na uwezo wa kutatua matatizo ndio wanaofanikiwa. Shule hutoa tahadhari, lakini maisha yemejikita kwenye kujaribu. Shule huwatunuku vizuri wale wote ambao wanafuata sheria, lakini maisha huwatunuku zawadi wale wote wanaothubutu kivunja sheria na kutengeneza mpya.

Kuongoza darasani hakumaanishi kuwa utaweza kufanya vizuri kwenye maisha nje ya darasa. Duniani kuna watu wengi ambao hawakufanya vizuri darasani lakini ni matajiri katika maisha kutokana na uwezo wao wa kuchangamkia fursa na kutatua matatizo.

Ni wazi kuwa katika nyakati hizi kuna wahitimu wengi waliomaliza vyuo lakini maisha yako hayaeleweki, huku wengine wakitembea na vyeti wakitafuta kazi ambazo hazipo kabisa. Vyeti havitakuwa suluhisho kwao, bali uwezo wao wa kuona fursa na kuzichangamkia utawaoko wasianguke katika dimbwi la umasikini ambalo tayari baadhi wameangukia humo.

Hapa chini ni sababu saba kwani wahitimu wa vyuo huishia kuwa masikini.

  1. HAWAFIKIRII NJE YA VYETI VYAO

Albert Eistein amewahi kusema kuwa elimu sio kujifunza kuhusu ukweli, bali ni kuifundisha akili namna ya kufikiri. Umewahi kusikia msemo “Fikiri Nje ya Boksi”. Moja ya sababu kubwa kwanini wahitimu wengi wanakuwa masikini ni kwa sababu hawawezi au hawataki kufikiri nje ya boksi.

Wapo waliohitimu uhandisi lakini wakafanya kazi benki. Kuna waliohitimu kozi ya udaktari lakini wana ujuzi mkubwa wa utengenezaji tovuti na graphics. Wapo wanasheria ambao ni wataalamu katika masuala ya fedha (uhasibu).

Ukweli ni kwamba ujuzi ambao unahitajika katika maisha kukuwezesha wewe kufanikiwa sio lazima upatikane ndani ya kuta nne za darasa. Vyeti vyako ni ushahidi tu kuwa ulikwenda shule na unafundishika, na havina uhusiano na kile ambacho una uwezo wa kukifanya. Una uwezo wa kufanya mambo mbalimbali, pale utakapoamua kufikiri nje ya shahada na vyeti vyako.

2. HUVIPA VYETI KIPAUMBELE KULIKO TALANTA NA VIPAJI WALIVYONAVYO

Ni muhimu ikaeleweka kuwa, hutakiwa kuacha kipaji au talanta uliyonayo wakati ukihangaika kutafuta kazi kupitia vyeti vyako. Lazima vitu hivyo vijazilizane, viende sambamba wakati ukikiendea kile unachokipenda au kutafuta kazi.

Kila mtu ana kipaji fulani, na kufanikiwa kwetu katika maisha kunatokea pale tu tunapokuwa na uwezo wa kivitambua vipaji vyetu na kuvifanyia kazi. Ili tuishi maisha mazuri na yenye matokeo mema ni lazima tutilie mkazo zaidi kwenye vipaji vyetu wakati mwingine kuliko hata kazi zetu. Tuvivumbue vipaji, tuviendeleze, na kuviuza katika huu ulimwengu. Usizike kipaji chako kwa kutumia vyeti ulivyopata.

3. VYETI VYAO HUWAANDAA KUIKABILI DUNIA AMBAYO HAIPO

Ni wazi kuwa, mafunzo au elimu ambayo inatolewa kwenye shule na vyuo kwa sasa, haina matumizi tena katika dunia ya sasa. Dunia imebadilika sana, hivyo na mahitaji ya watu yamebadilika. Ni wazi kuwa elimu inayotolewa katika vyuo vingi haiwaandai wanafunzi kwa maisha yajayo.

Wahitimu wanakuwa viumbe waliopo hatarini katika dunia ya leo ambayo inabadilika kwa kasi. Vyuo vimejazwa na wahadhiri ambao wana mfumo wa kufundisha ambao hawabadiliki, maelezo ya kufundisha ni yale yale kila mwaka, mbinu ni zile zile, jambo ambalo halina tena nafasi kalika miaka ya sasa.

4. HAWAJITAMBUI WAO, LAKINI WANAFAHAMU ZAIDI KUHUSU VITU

Vyeti haviwawezeshi watu kujitambua  kwamba wao ni watu wa namna gani, zaidi huonesha uwezo wa akili yetu. Mtu masikini ni mtu ambaye hajajitambua bado. Kwa kwadiri utakavyoweka juhudi katika kuweza kujitambua, namna utakavyoweza kutambua hazina iliyofichwa ndani mwako, utaweza kufanikiwa.

Kila mmoja ndani yake ana kitu cha muhimu sana ambacho kitaweza kutoka nje na kuiangaza dunia pale atakapoweza kukitambua, kwani hakuna mtu mwingine anayeweza kukiona, bali wewe mwenyewe.

5. VYETI NA SHAHADA HUWEZA KUUA JITIHADA

Vyeti na shahada uliyoipata vinaweza kutumika kufunga akili yako punde fursa zinapojitokeza mbele yako. Ni vyema kuwa makini kuhakikisha kuwa viwili hivyo haviifungi akili yako. Lengo la elimu ni kuifungua akili yako kuweza kuona fursa lukuki zinazokukabili.

Fred Smith aliona fursa katika kutoa huduma ya kusafirisha vitu nyakati za usiku nchini Marekani, na pia kusafirisha sehemu yoyote duniani, na hivyo kupelekea kuzaliwa kwa kampuni ya FedEx. Cha kushangaza ni kuwa Fred Smith alipata daraja ‘C’ katika somo la uchumi kwenye chuo cha Yale, kutokana na kutoa wazo ambalo mkufunzi wake, Profesa, alisema kuwa halitekelezeki.

Kampuni yake ilikuwa kampuni ya kwanza ya Marekani kupata faida zaidi ya dola 10 bilioni kwa mwaka. Katika usiku wa kwanza, kampuni hiyo ilisafirisha vifurushi 186, lakini kwa sasa FedEx sasa inasafirisha vifurishi karibu nchi zote duniani, ikitumia ndege zaidi ya 6,030, magari 46,000 na wafanyakazi 141,000.

6. SHAHADA NA VYETI VINAKUFANYA UTAFUTE KAZI NA SIO FURSA

Vyeti na shahada tunazopata baada ya kuhitimu masomo yetu vinatufanya tuwe watafutaji wa kazi badala ya kuangalia fursa ambazo zinaweza kubadilisha maisha. Wewe si maskini kwa sababu huna kazi, bali ni maskini kwa sababu huzioni fursa na kuzitumia.

Kunachowafanya baadhi ya watu kupata maendeleo zaidi ya wengi, mara nyingi sio vyeti vyao bali huitumia elimu waliyoipata na kufungua akili zao kuweza kuona fursa mbalimbali na kuzichangamkia. Kwa vile kila mara kuna tatizo linalohitaji ufumbuzi, fursa hazitokoma. Itakuwa ni suala la kupoteza muda, elimu na uzoefu ulioupata kama baada ya kuhitimu chuo, utakachokuwa unakiwaza ni kutafuta kazi.

7. SHAHADA HUWAANDA WATU KUTAFUTA SEHEMU SALAMA NA SIO KUWA NA UTHUBUTU

Elimu ambayo inatolewa kwa sasa, inawaandaa wahitimu kutafuta sehemu salama ya kukaa (kazi rasmi) na sio kuwa watu wenye uthubutu wa kujaribu, waliopo tayari kukosea na kujaribu tena. Kujaribu na kujifunza kutokana na makosa yetu kunatusaidia kufahamu kipi kinawezekana na kipi hakiwezekani.

Thomas Edison aliyegundua balbu ya umeme alipoulizwa kwamba anajisikiaje kwamba alishindwa mara 999 kuunda balbu hiyo, hadi mara ya 1000 ndipo alipofanikiwa, alijibu kuwa, hakushindwa mara 999, bali alijifunza mara 999 kutengeneza balbu inayowaka.

Wahitimu wengi wanaendelea kuwa maskini kwa sababu ujuzi unaohitajika kuwawezesha kutajirika haufundishwi katika vyuo. Hadi kufikia mwaka 2025, jumla ya ajira milioni 5 ambazo sasa zinafanywa na watu, zitakuwa zinafanywa na mashine.

Ajira za kipindi hicho zitahusu uzalishaji wa maarifa, ubunifu, na watu ambao watakuwa na ujuzi unaopatikana darasani pekee, hawatafaa katika dunia inayobadilika. Vitu kama ufikiri wa kina, ubunifu, ujuzi wa tabia za watu, utatuzi wa matatizo, utaalamu wa mifumo ya kompyuta, ndivyo vitakuwa na tija zaidi wakati huo.

HITIMISHO, ni muhimu kwa wanafunzi waliopo kwenye ngazi mbalimbali za kielimu kufikiri zaidi nje ya boksi. Jitolee kufanyakazi hata bila malipo na pia usiogope kufanya kazi katika fani tofauti na uliyosomea. Kufanikiwa kwako kutakuhitaji kuweza kufahamu vitu mbalimbali ili utakapoviweka pamoja uweze kutatua matatizo.

Anza sasa kusoma vitu mbalimbali ambavyo vinakuvutia. Ukiwa chuoni, soma kozi mbalimbali hata kama hazihusiani na kozi kuu unayoisoma, amini, vitu hivyo vitakusaidia huko mbeleni.

Usijifungie tu darasani, fanya vitu vingine. Gombea nafasi za uongozi, hata kama utashindwa lakini utajifunza kitu ambacho darasani mwalimu wa somo la siasa hatafundisha, anzisha biashara hata kama itafeli, hiyo ni sehemu ya ujasiriamali. Hudhuria semina, soma vitabu nje ya fani yako.

Usiwaze sana kuhusu kuwa mwanafunzi bora, japo ukiwa ni jambo bora, lakini fikiri zaidi juu ya kuwa mtu bora. Usifanye darasa kuwa dunia yako, bali ifanye dunia kuwa darasa lako. Jaribu vitu vipya, wekeza juu ya kile unachokiamini. Usalama na uhuru wa kifedha haupo katika kazi yako, lakini katika kipaji chako, ubunifu wako na uwezo wako wa kuona fursa na kuzinyakua.

Send this to a friend