Mambo ya kufahamu kuhusu Dkt. Sengati ambaye uteuzi wake umetenguliwa leo na Rais Samia

0
50

Leo Oktoba 8, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Dkt. Philemeon Sengati, ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Tuiangazie kwa ufupi safari ya Dkt. Sengati hadi alipofika Shinyanga.

Mei 15, 2021 mkoa wa Shinyanga ulimpata mkuu mpya wa mkoa, Dk. Sengati, baada ya kudumu kwa miaka mitano na Zainab Telack aliyeuongoza mkoa huo tangu mwaka 2016, akipandishwa cheo kutoka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema.

Dk. Sengati aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika mabadiliko ya safu ya viongozi wakuu wa mikoa.

Dk. Sengati kabla ya uteuzi huo  alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, nafasi aliyoitumikia kwa miezi 10, kuanzia Julai 3, 2020 akirithi mikoba ya Aggrey Mwanri. Aliteuliwa na Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk. John Magufuli kuchukua mikoba ya Mwanri ambaye alistaafu.

Kabla ya uteuzi huo wa kuwa RC wa mkoa wa Tabora, Dk. Sengati alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Magu, Dk. Sengati alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma akiwa idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, akifundisha programu za International Relations, Critical Thinking and Argumentation pamoja na Conflict Management.


Kati ya 2009-2014 alisoma na kuhitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma akibobea katika Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma

Kati ya 2002-2004 alisoma na kuhitimu Shadaha ya Umahiri (Masters) katika Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma akibobea katika Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwaka 1998-2001 alisoma na kuhitimu Shahada ya Awali katika Sayansi ya Siasa akijikita kwenye Falsafa (Philosophy) kutoka The Affiliated Urbaniana University kilichopo Rome nchini Italia.

Elimu ya sekondari (pamoja na kidato cha tano na sita) alipata kutoka St. Pius Makoko Seminary iliyopo Musoma kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 1997.

Alipata elimu ya msingi kutoka Shule ya Msingi Sima iliyopo Sengerema mkoani Mwanza kuanzia mwaka 1984 hadi mwaka 1990.

Pia amepata mafunzo mbalimbali kwa ngazi ya cheti kutoka Tanzania na Kenya.

Send this to a friend