Kikundi cha G20, au Kundi la Mataifa 20, kinajumuisha nchi 20 zenye uchumi mkubwa duniani na kinatambulika kama jukwaa muhimu kwa majadiliano ya masuala ya kiuchumi na kifedha ya kimataifa. Kiliundwa mwaka 1999 kama jibu kwa mgogoro wa kifedha uliotokea Asia ya Mashariki mwishoni mwa miaka ya 1990. Lengo la awali lilikuwa kujadili masuala ya kifedha na uchumi, lakini baadaye likaongeza wigo wake kujumuisha masuala mengine ya kimataifa kama mazingira, usalama wa mtandao, na maendeleo endelevu.
Nchi wanachama wa G20 zina uwakilishi mkubwa katika idadi ya watu duniani na uchumi wa kimataifa. Wanachama hawa ni Argentina, Australia, Brazil, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japan, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Korea Kusini, Uturuki, Uingereza, Marekani, na Jumuiya ya Ulaya.
Viongozi wa nchi wanachama wa G20 hukutana kila mwaka. Mkutano huu ni fursa kwa viongozi hao kujadili masuala ya kiuchumi, kifedha, na kisiasa, na kufikia makubaliano kuhusu sera na mikakati ya kimataifa.
G20 ina ajenda ya kazi ambayo inajumuisha masuala mbalimbali ya kimataifa. Kwa mfano, masuala kuhusu ukuaji wa uchumi, ajira, biashara, mazingira, elimu, afya, na usalama wa kimataifa yanaweza kujadiliwa katika mkutano huo. Lengo ni kutafuta njia za kushughulikia masuala hayo kwa ushirikiano.
Mbali na hayo, G20 inaweza kutoa mwongozo kwa sera za kiuchumi na kifedha ulimwenguni kote na kusaidia kutatua migogoro ya kiuchumi. Pia, inaweza kuchangia katika juhudi za kimataifa za kushughulikia masuala ya dharura kama mabadiliko ya tabianchi na usalama wa kimataifa, miongoni mwa mengine.
Kila nchi mwanachama wa G20 inawakilishwa na kiongozi wake wa juu, ambaye ni Rais au Waziri Mkuu. Pia kuna mikutano ya mawaziri wa fedha, mawaziri wa mambo ya nje, na wataalam wa sera za kiuchumi na kifedha.
India ndiye mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu, ambapo ajenda kuu imejikita katika mjadala kuhusu utoaji wa mikopo zaidi kwa mataifa yanayoendelea kutoka taasisi za kimataifa, marekebisho ya muundo wa madeni ya kimataifa, na athari za kutokuwa na uhakika wa kijiografia kwa usalama wa chakula na nishati.