Mambo ya kuzingatia wakati wa kufungua biashara yako baada ya mlipuko wa corona

0
36

Na Kai Mollel

Mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu (Covid-19) umeathiri na unaendelea kuathiri sekta za kijamii na kiuchumi dunia nzima. Kutokana na ripoti ya UNDP Tanzania 2020 sekta zitakazoathirika zaidi ni kama utalii, usafirishaji na uchuuzi.

Kwa wafanyabishara wa kati na wadogo (SMEs) pamoja na wajasiriamali athari za Covid-19 zimezopelekea kufunga au kusimamisha au kupunguza kasi ya biashara zao.

Sasa katika kujiandaa na maisha baada ya corona inabidi ifanyike tathmini na kujipanga. Ni muhimu kufanya tathmini ya kina ya mwenendo wa biashara yako kabla na kipindi cha #COVID19 na kufanya makisio itakuwaje baada ya #COVID19.

Mambo ya msingi ya kuangazia wakati wa tathmini ni;

1. Kama biashara ilikua inafanya vibaya kabla ya #COVID19 na inaendelea kufanya vibaya kipindi cha #COVID19, ni muhimu kuanza kufikiria namna mpya ya ufanyaji wa biashara ama kufikiria wazo jipya.

2. Kama biashara yako ilikuwa inafanya vizuri kabla ya corona na kipindi cha corona inafanya vibaya, Tathmini uwezekano wake kustahimili kipindi hichi na njia za kuiimarisha iweze kuendelea kwa mikakati ya kupunguza garama na kupanua wigo wa soko.

3. Kama biashara yako ilikuwa inafanya vibaya kabla ya corona na Kipindi cha corona inafanya vizuri, tafuta njia za kuiendeleza, kuikuza na kuimarisha zaidi. Kifupi ni, weka nguvu pale panapotoa matokeo chanya, ili upate matunda zaidi.

Baadhi ya njia za kuendeleza, kukuza na kuimarisha biashara kipindi cha corona na baada ya kipindi hicho;

1. Kiini cha biashara ni watu. Watu ambao ni wateja wako, watu wanaokufanyia, unaofanya nao kazi pamoja na watu wanaokuzuguka. Kwa hiyo, ili kurudi ktika kazi lazima tuanze kufikiria usalama wa kiini hiki.

2. Tengeneza mikakati mipya ya kazi na mifumo inayoakisi hali hii mpya ya corona, hii ni kuanzia kwenye ubunifu wa wazo mpaka jinsi unavyoiendesha biashara yako.

3. Tengeneza mikakati ya kurudi kwa awamu huku ukiangalia hali zisizotarajiwa, kwa sababu hali ni tete hushauriwi kurudi mzima mzima. Jipange ni kipi na wapi na vipi unaanza.

4. Wasiliana na wote walioko katika mnyororo wako wa thamani kuhusu mipango yako na kuwa mkweli kuhusu hali yako na utayari wa kuendelea kufanya kazi nao. Wasiliana na wateja wape taarifa ya kufungua tena.

5. Kanuni ya jumla ni “pesa ni mfalme” kwa hiyo kama una fedha taslimu (mkononi) jitahidi unavyoweza kubaki nazo kadri inavyowezekana. Unapofanya makadirio ya mipango na matumizi kuwa na mipango ya pale hali itakapokua mbaya zaidi.

6. Ili wateja ulionao waendelee kuja kwako na wapya wakufuate toa thamani zaidi. a) Fikiria mbinu mpya za kufikisha huduma kwa wateja, b) Njia rahisi za malipo ya mtandao ama kwa simu na c) Pendezesha ofisi yako ya mitandaoni iwe inajitegemea kumhudumia mteja.

“Tusitumie muda mwingi kujaribu kurudisha hali ya mambo kuwa kama ilivyokua kabla ya #COVID19. Ni vizuri tujikita zaidi katika kutazama fursa mpya za hali hii tuliyonayo hivi sasa,” ameandika Mollel.

Send this to a friend