Mamlaka yaeleza sababu za mashabiki wenye ‘N-Card’ kuzuiwa kuingia uwanjani

0
49

Kutokana na kadhia mbalimbali zinazojitokeza katika baadhi ya mechi mbalimbali kubwa hususani za Simba na Yanga ambapo mashabiki husalia nje ya uwanja wakiwa na tiketi zao mkononi huku wakiambiwa uwanja umejaa, suala hili limekuwa likizua mijadala tofauti huku wengine wakizilaumu klabu husika.

Kuendelea kujirudia kwa kero hii kumetufanya kuzungumza na wahusika wa mfumo wa ukataji wa tiketi za kielektroniki (N-CARD) ambao wamesema kuna makundi mawili ya tiketi zinazotolewa; makundi hayo ni tiketi zinazotolewa na uwanja husika na kuwekwa kwenye mfumo wa N- Card kwa idadi maalum ambazo wao ndio hushughulika nazo na tiketi zinazotolewa na klabu mwenyeji vinavyohusika na mchezo.

Akitolea ufafanuzi Meneja wa Oparesheni N-Card, Nasra Mohamed amesema moja ya mambo yanayochangia watu kukosa nafasi za kuingia uwanjani ni pamoja wizi unaofanyika ambapo baadhi ya watu huuziwa kadi ambazo hazina tiketi.

“Kuna watu ambao wanakuwa na kadi za N-Card hazina tiketi halafu wanaziuza pale nje ya uwanja nao hao pia wanakuwa wanawaibia mashabiki, wananunua wakifika pale wanakuta kadi haina tiketi, sasa yule shabiki mpaka aelewe kwamba ameibiwa kwa sababu yeye ametoa pesa yake halali atasema kwamba mimi nina kadi na ina tiketi lakini kiuhalisia ndani haina tiketi,” ameeleza.

Ameongeza kuwa “ili uweze kupita pale [getini] si kwamba uwe na kadi tu, unatakiwa uwe na kadi ambayo imenunuliwa tiketi ya halali na haijatumika ndo uweze kupita pale.”

Amegusia chanzo kingine kuwa ni kundi la watu wenye ulemavu na watoto ambao wanaingia na wazazi wao ambao hawalipii kuingia uwanjani, hivyo baadhi ya nafasi hujazwa na watu hao na kupelekea baadhi wenye tiketi halali kukosa nafasi.

Msanii aitaka kampuni ya mabasi imlipe milioni 123 kwa kutumia wimbo wake

Kwa upande wa mechi ya Yanga SC na ASAS FC katika uwanja wa Azam Complex, Nasra amedai uwanja huo haujulikani idadi kamili ya watu wanaopaswa kuingia uwanjani kwa kuwa uwanja hauna viti maalum.

“Uwanja wa Azam mzunguko hauna viti una mabenchi kwa hiyo uhalisia wa namba exactly wangapi wanakaa kwenye ule uwanja hakuna mtu anayejua. Pia sababu nyingine ni kuwa kuna baadhi ya benchi zilikuwa haziko salama watu hawawezi kukaa, kwahiyo idadi kamili ya mzunguko itazamwe ili ijulikane idadi kamili, hiyo pia inaweza kuwa imechangia kwa uapande wa jana,” ameongeza.

Amehitimisha kuwa N-Card inashirikiana na Jeshi la Polisi, TAKUKURU na vilabu ili kuwakamata watu wanaowauzia watu tiketi ambazo si halali na kuwafikisha kwenye vyombo husika, pia ameshauri vilabu kuwashawishi mashabiki kununua tikieti kwenye vituo maalum ili kuepuka kuibiwa na kuongeza kuwa tayari imezungumza na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) na vilabu kutafuta namna ya kusimamia makundi maalum yanayoingia uwanjani ili kuwa na utaratibu maalum.

Send this to a friend