Mamlaka zakana kuitambua dawa ya COVIDOL inayodaiwa kutibu Corona

0
33

Dawa iliyopewa jina la COVIDOL inayodaiwa kutibu ugonjwa hwa homa ya mapafu (COVID-19) unaosababishwa na virusi vya corona imeleta mtafaruku baada ya taarifa zake kusambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) ambalo ndilo linalozalisha dawa hiyo, limesema ni kweli dawa hiyo imeonesha kuwasaidia sana watu wenye maambukizi ya ugonjwa huo.

“Baada ya kuitengeneza tumeiwasilisha kwenye mamlaka ya serikali, imepimwa na imeonekana ina ubora na ni salama kwa matumizi ya binadamu,” amesema Prof. Hamis Malebo ambaye ndiye mgunduzi wa dawa hiyo wakati akifanya mahojiano na TBC.

Licha ya TIRDO kukiri kuwa imezalisha zaidi ya chupa 900 hadi sasa, mamlaka mbalimbali za serikali zimesema haziitambui dawa hiyo na kwamba zimeiona tu kwenye mitandao ya kijamii.

“COVIDOL na mimi nimeiona kwenye mitandao ya kijamii, bado haijafika NIMR [Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu],” imesema taasisis hiyo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na Tiba Mbadala katika Wizara ya Afya, Dkt. Paul Mohammed amesema dawa hiyo haijathibitishwa na wizara hiyo, hivyo kuonekana kwake kwenye mitandao ya kijamii isichukuliwe kwa imethibitishwa.

Hata hivyo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ilikataa kuonesha ushirikiano walipoombwa kutoa maelezo kuhusu dawa hiyo.

Wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari kuhusu dawa mbalimbali zinazosambazwa mitandaoni kwa maelezo kuwa zinatibu magonjwa mbalimbali ikiwamo corona.

Send this to a friend