Aliyekuwa Msemaji wa Klabu ya Yanga, Haji Manara amemwomba radhi Waziri wa Michezo, Mohamed Mchengerwa kwa kudhania kuwa amelielekeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kumfungia kujishughulisha na shughuli za mpira ndani na nje ya nchi.
Manara amedai kumekuwa na kutokuelewana baada ya vyombo vya habari na mitandao kuripoti kuwa ‘Waziri amemshukia Manara’ na kwamba taarifa hizo zilimfanya aingie ‘kichwa kichwa’ na kumtupia lawama.
“Katika maelezo yangu na mimi nikajikosea, nikaikosea Serikali, nikamkosea na waziri mwenyewe kwamba kuonesha Waziri alitoa maelekezo kwa TFF, lakini baadaye nikaja kufuatilia baada ya kuzungumza na baadhi ya maafisa wa wizara, wakanihakikishia kwamba hiyo ni standard ambayo ameiset waziri toka alipokuwa Waziri wa Michezo,” amesema Manara.
Ameongeza, “amekuwa akizungumzia suala la maadili na nidhamu kwa viongozi na taasisi zenyewe, nikaona kwamba mazungumzo yake pale kwenye siku ya tuzo hayakujikita kwenye jambo langu, na ni jambo jema alilokuwa analifanya Waziri,”ameeleza Manara.
Julai 21, 2022 Kamati ya Maadili ya TFF, ilimfungia Haji Manara kutojihusisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi kwa miaka miwili pamoja na faini ya TZS milioni 20 kwa kosa la kumtolea maneno yasiyofaa Rais wa TFF, Wallace Karia katika mechi ya fainali ya kombe la Azam iliyochezwa Jijini Arusha.