Manara: Nisingetamka maneno yale kama nisingechokozwa

0
39

Kamati ya Maadili ya TFF imemfungia Msemaji wa Klabu ya Yanga, Haji Manara kujihusisha na soka ndani na nje ya nchi kwa miaka miwili na kutozwa faini ya shilingi milioni 20.

Manara amefungiwa kwa kosa la kumkashifu Rais wa TFF, Wallace Karia katika fainali ya kombe la shirikisho la FA iliyofanyika jijini Arusha.

Kamati imejiridhisha baada ya video iliyomuonesha Manara akikiri kufanya kitendo hicho na kuomba msamaha kwa Rais wa TFF, waandishi na wadau wa michezo.

Pia alikiri kitendo alichokifanya hakikuwa cha kistaarabu na kinaleta taswira mbaya kwa mpira wa Tanzania.

Aidha, Kamati imeeleza kuwa katika utetezi wake wa maandishi mlalamikiwa alisema yeye si kichaa hivyo hawezi kutamka maneno yale mbele ya watu bila kuchokozwa.

Manara aliendelea kusema, hakukuwa na kutukanana bali ni kutofautiana kidogo na maneno yake hayawezi kuwa vitisho au kumzuia Rais kutimiza maneo yake hivyo, si haki kumshtaki kuwa amemkashifu na wala maneno yake hayakuwa ya kuuzi.

Kamati imesema kitendo alichokifanya vilihatarisha amani na kupelekea polisi kuigilia kati.

“Kwa ujumla vitendo alivyovifanya mlalamikiwa siku ya mechi vilichangia katika kusababisha vurumai uwanjani ambavyo vilisababisha polisi kuingilia kati kwa kufyatua mabomu ya machozi, vurugu hizo zingeweza kuleta madhara makubwa sana kama isingekuwa polisi kuingia kati,” Walter Lungu, Katibu Kamati ya Maadili TFF.

Hata hivyo, kamati imesema adhabu hiyo itaanza kutumika kuanzia leo Julai 21 na haki ya kukata rufaa iko wazi.

Send this to a friend