Mange Kimambi ashtakiwa kwa kutakatisha fedha, adai Serikali inapanga kumrejesha nchini

0
87

Mwanaharakati Mange Kimambi anayeishi nchini Marekani amefunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi nchini Tanzania, akidaiwa kutakatisha TZS milioni 138.5.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyowasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mnamo Agosti 28, 2025, Mange anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 1 na Machi 31, 2022. Upande wa mashtaka unadai kuwa fedha hizo ni mapato yatokanayo na uhalifu.

Kesi hiyo, iliyosajiliwa kama Kesi ya Jinai Na. 000021172/2025, imepangwa kutajwa Desemba 4, 2025, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hassan Makube.

Hati ya mashtaka inaeleza kuwa Mange alijipatia kiasi hicho cha fedha kwa kufanya kazi ya uandishi wa habari bila kupata kibali pamoja na kudai fedha kupitia vitisho. Kosa hilo linatajwa chini ya Sheria ya Udhibiti wa Utakatishaji Fedha, ikisomwa pamoja na Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi na Uhalifu wa Kujumuika.

Akijibu tuhuma hizo kwenye mitandao yake ya kijamii, Mange ameeleza kuwa Serikali imepanga kumrejesha nchini ili kukabiliana na tuhuma hizo.

Hadi sasa, haijafahamika iwapo hatua za kimataifa zinazodaiwa zimeanza kuchukuliwa, huku wadau mbalimbali wakifuatilia mwenendo wa kesi hiyo ambayo imezua mjadala mpana mtandaoni.

Send this to a friend