Mangula: Bagamoyo tuliahidi kujenga gati sio Bandari

0
42

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula amewataka Watanzania kutohangaika na upotoshaji unaofanya na baadhi ya watu mitandaoni kuhusu ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, na kwamba wamuache Rais Samia Suluhu Hassan afanye kazi yake ya kutekeleza mipango ya maendeleo.

Amesema hayo akizungumzia ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani ambapo amebainisha kuwa bandari hiyo haijapitishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya 2020-2025, hivyo hakuna sababu ya kuwapotosha wananchi, badala yake waunge mkono utekelezaji wa miradi iliyoahidiwa.

“Nashangaa huu mjadala unatokea wapi kwa kuwa mradi huo haupo. Hakuna haja ya watu kupotosha wananchi,” amesema Mangula akizungumza na Gazeti la Uhuru na kueleza kwamba kilichoahidiwa ni ujenzi wa gati ya Bagamoyo.

“Ipo miradi ya maboresho ya bandari, lakini kwa upande wa Bagamoyo kilichopitishwa ni ujenzi wa gati, sio bandari,” amesema Mangula.

Juni mwaka huu akizungumza na wafanyabiashara, Rais Samia Suluhu Hassan aliweka wazi kuwa serikali imeanza mazungumzo ya kufufua mradi wote wa bagamoyo ambao unajumuisha bandari na eneo la maalum la uwekezaji.

Akiwa madarakani, Hayati Rais John Magufuli alikataa kuendeleza mradi huo ambao mkataba wake ulisainiwa wakati wa uongozi wa mtangulizi wake, Rais Dkt. Jakaya Kikwete, kwa maelezo kwamba masharti yake hayakuwa rafiki na kwamba yangeliingiza Taifa matatizoni.

Send this to a friend