Maombi ya Halima Mdee na wenzake 18 kusikilizwa leo

0
98

Maombi ya kibali cha kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama yaliyowasilishwa na Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Halima Mdee na wenzake 18, inatarajiwa kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Shauri hilo ambalo litasikilizwa mbele ya Jaji Mfawidhi, John Mgeta lilifunguliwa na wabunge hao dhidi ya bodi ya wadhamini ya CHADEMA wakipinga kuvuliwa uanachama uliofanywa na baraza kuu la chama hicho.

Wajibu maombi wengine ni Tume ya Uchaguzi (NEC) pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambao watawakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata.

Aidha, bodi ya wadhamini ya CHADEMA itawakilishwa na Wakili Peter Kibatala huku Halima Mdee na wenzake wakiwakilishwa na Wakili Aliko Mwamanenge.

Halima Mdee na wenzake walivuliwa uanachama Mei 12 mwaka huu baada ya baraza kuu la CHADEMA kutupilia mbali rufaa waliyokata wabunge hao kupinga kuvuliwa uanachama na kamati kuu ya chama hicho.

Send this to a friend