Mapacha wafariki baada ya nyumba kuteketea Iringa

0
46

Mapacha wa mwaka mmoja wamefariki baada ya nyumba yao kuteketea kwa moto katika Kijiji cha Magulilwa wilayani Iringa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema tukio hilo limetokea Julai 30, mwaka huu ambapo pacha hao Eliza na Erick Msigwa walipoteza maisha yao kwa nyakati tofauti, mmoja akipoteza maisha wakati nyumba inateketea, na mwingine wakati akikimbizwa hospitalini.

Aidha, mama wa watoto hao, Warda Msisi amesema kabla ya kufikwa na mauti aliwalaza watoto wake ndani ya nyumba hiyo kisha akaenda dukani kununua sabuni, wakati anarudi nyumbani ndipo alikuta tukio hilo.

“Duka lenyewe haliko mbali na sikuchukua muda mrefu, nilipokuwa narudi nilishangaa kuona watu wamekusanyika nyumbani kwangu, nikaona moshi kumbe nyumba inaungua,” amesema.

Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kubaka na kuua

Ameongeza, “nilishtuka kwa sababu watoto walikuwa ndani lakini nikawa nimechelewa, mmoja alikauka kabisa na mwingine alikuwa bado hai ila naye aliniacha. Sina kingine kinachoniumiza ni hawa watoto tu, sielewi ilikuwaje na sijui chanzo cha moto ni nini hadi sasa.”

Watoto hao wamezikwa Julai 31, 2023 kijijini kwao Magulilwa, huku Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.