Mapendekezo 10 ya ACT Wazalendo Ripoti ya CAG 2021/22

0
31

Chama cha ACT-Wazalendo leo Aprili 10, 2023 katika mkutano na vyombo vya habari kimetoa mapendekezo kwa Serikali kutokana na ripoti iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Haya ni mapendekezo 10 yaliyotolewa na chama hicho;

1. Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF)

“Mfumo unaotumika haufanyi NHIF kuendelea kupata mapato mengi ambayo yanaweza kuhudumia watu wengi.

Tunapendekeza kufanya mabadiliko makubwa kwenye mfumo mzima wa bima ya afya nchini, tunataka suala la bima ya afya lifungamanishwe na hifadhi ya jamii, kwa hiyo tunapendekeza yafuatayo;

-“Mifuko wa hifadhi ya jamii NSSF na PSSSF iwe na fao la matibabu ambalo kila mwanachama wa mifuko hiyo awe moja kwa moja ni mwanachama wa mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa.”

-“Wanaochangia NSSF na PSSSF asilimia 20 ya michango ya wanachama hao kwenye hiyo mifuko iwasilishwe NHIF kila mwezi kwa ajili ya kugharamia fao la matibabu.”

-“Serikali iwalipe kwa asilima 100 wanufaika wa TASAF kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii hivyo watakuwa moja kwa moja ni wanachama wa NHIF.”

-“Tunaishauri Serikali itenge bajeti kila mwaka asilima 2.5 ya pato la taifa kwa ajili ya kugharamia matibabu na hivyo kuwezesha watu milion 11 kuwa na bima ya afya pamoja na wategemezi wao.”

-“Bodi na menejimenti yote ya NHIF ibadilishwe.”

-“Pia tunapendekeza muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote uandikwe upya ikizingatia mapendekezo yetu na sheria mpya ya NHIF itungwe ili kuimarisha mfumo wa huduma ya bima ya afya nchini.”

2. Deni la taifa

“ACT-Wazalendo tunaitaka Serikali kufanya mapitio ya mikataba yote ya mikopo ili kufuta mikataba ambayo haitekelezeki na ile inayotekelezeka ipokee fedha na kutekeleza malengo kusudiwa.”

3. Upotevu wa fedha za mikopo

“Tunapendekeza mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu itolewe kupitia skimu za uhifadhi wa jamii ambapo fedha hizi zitakuwa ni mchango wa mamlaka za serikali za mitaa kwa wananchi wenye sifa watakaoingia kwenye skimu husika.”

4. Matumizi mabaya ya fedha za mkopo za UVIKO-19

“Tunaitaka Serikali kuwachukulia hatua watu wote waliohusika katika ubadhirifu wa fedha za UVIKO-19.”

5. Usimamizi wa mradi wa Bwawa la Nyerere

“Waziri wa Nishati na Waziri wa TAMISEMI wahakikishe makubaliano yaliyofikiwa ya mkataba yanatekelezwa kuanzia mwaka huu wa fedha Julai 2023.”

“Tunataka Serikali ichukue hatua kwa watendaji wote waliohusika kwenye uzembe wa kupoteza fedha za mradi.”

CHADEMA: Waziri Mkuu awajibike kwa ripoti ya CAG

6. “Mradi wa DART awamu ya pili

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) ambaye ndiye msimamizi mkuu wa mradi huu kuchukua hatua stahiki dhidi ya mkandarasi wa mradi.”

“Mshauri mwelekezi wa mradi huu afukuzwe kazi.”

“Matumizi ya gesi asilia yakitumika kuendesha mabasi yatakata gharama za uendeshaji za Shirika, hivyo yatapelekea watumiaji kupunguziwa nauli kuliko nauli ya sasa.”

7.Shirika la ndege ATCL

“ACT- Wazalendo inapendekeza Serikali kuirejesha Wakala wa Ndege za Serikali (TFGA) kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ili mamlaka za juu ziweze kusimamia hao wa chini.”

“Tunapendekeza CAG afanye ukaguzi maalum wa manunuzi ya ndege tangu tulipoanza kununua ndege mwaka 2016.”

8.Ujenzi wa Reli (SGR)

“Bunge liunde kamati teule ya Bunge ichunguze sababu za bei ya manunuzi ya treni kuongezeka na mapendekezo ya bunge ya hatua mahususi ya kuchukua.”

“Kamati ya bunge iwahoji Standard Chartered Bank ya Uingereza kuhusu masharti ya kulazimisha ukandarasi wa kujenga reli.”

 

9. Vishkwambi vya sensa

“Baada ya kuthibitsha kuwa Waziri wa Miundombinu, Profesa Makame Mbarawa aliwaongopea wabunge kwa kusema uongo bungeni, tunamtaka Waziri Mbarawa awajibike kwa kujiuzulu na kuliomba radhi bunge.”

10. TANROAD

“Tunamtaka Mkurugenzi Mkuu wa TANROAD ajiuzulu nafasi yake, ama Rais [Samia Suluhu] amfukuze kazi mara moja kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.”

“Tunashauri mamlaka za juu za nchi zitafakari kama ni sahihi kuendelea kuunganisha Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi.”

Send this to a friend