Mapinduzi ya Kijeshi Afrika: Kwanini Majenerali huishia Ikulu?

0
5

Katika miaka ya hivi karibuni, Afrika imeshuhudia wimbi la mapinduzi ya kijeshi likivuma kutoka Afrika Magharibi hadi Kati. Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kuwa baadhi ya viongozi wa mapinduzi hayo, waliokuwa awali wakiahidi mpito wa muda mfupi, wameishia kugombea au kushika rasmi nafasi ya urais, na hivyo kuleta maswali mengi kuhusu uhalali wa mabadiliko hayo.

Katika miaka ya karibuni, mifano ya wazi ya wanajeshi walioingia kwa nguvu na baadaye kuwa marais au kuonesha nia ya kugombea nafasi hiyo imeongezeka:

1. Mali – Koloneli Assimi Goïta
Mwaka 2020, Goïta aliongoza mapinduzi dhidi ya Rais Ibrahim Boubacar Keïta. Baada ya kipindi kifupi cha mpito kilichoongozwa na raia, alirejea tena madarakani kwa mapinduzi ya pili mwaka 2021 na kujitangaza kuwa Rais wa mpito. Goïta ameendelea kushikilia madaraka huku uchaguzi ukisogezwa mbele mara kwa mara.

2. Guinea – Luteni Kanali Mamady Doumbouya
Septemba 2021, Doumbouya alipindua serikali ya Rais Alpha Condé, akiahidi kurejesha utawala wa kiraia. Hata hivyo, alijitangaza Rais wa mpito na hadi sasa hakuna uchaguzi uliofanyika.

3. Gabon – Jenerali Brice Oligui Nguema
Agosti 2023, baada ya uchaguzi wenye utata, Oligui Nguema alipindua utawala wa Ali Bongo. Alichukua nafasi kama kiongozi wa mpito huku akisisitiza kuwa hatawania urais. Ngoema amegombea na kuchaguliwa kuwa Rais wa Gabon.

Kwanini wanajeshi wanaingia kwenye Urais baada ya Mpito?
Uungwaji mkono: Katika baadhi ya nchi, wananchi wameunga mkono mapinduzi, hasa baada ya kuchoshwa na tawala za muda mrefu au zisizowajibika. Wanajeshi hutumia hali hiyo kujijengea umaarufu wa kisiasa.

Kukosekana kwa vyama imara vya siasa: Hali hii huwapa nafasi wanajeshi kujijenga kama viongozi wa kisiasa bila ushindani mkubwa.

Nguvu ya madaraka: Baada ya mapinduzi, wanajeshi hushikilia vyombo vyote vya dola, usalama, fedha, na mawasiliano na hivyo kuwa na ushawishi mkubwa kuliko wanasiasa wa kiraia.

Kutaka Madaraka: Ahadi za mpito mara nyingi huchukuliwa kama njia ya kupooza jamii, lakini nyuma ya pazia huwa ni maandalizi ya kubaki madarakani.

Mitazamo ya wananchi na asasi za kiraia ni ipi?
Baadhi ya mataifa, wananchi wamekuwa wakiunga mkono mapinduzi kwa shangwe, wakiamini ni fursa ya kurekebisha mifumo iliyooza. Hata hivyo, matumaini hayo yamekuwa yakififia kadri wanajeshi wanavyoshikilia madaraka kwa muda usiojulikana.

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, kama chombo cha kikanda chenye jukumu la kudumisha amani, usalama, na utawala wa kidemokrasia katika Afrika Magharibi, imekuwa mstari wa mbele kulaani mapinduzi ya kijeshi yanayovunja utaratibu wa kikatiba.

Hata hivyo, Baadhi ya nchi wanachama wa ECOWAS wenye ushawishi wamekuwa wakishindwa kufikia kauli moja juu ya mapinduzi. Hii imesababisha kutokuwa na msimamo thabiti wa maamuzi yao.