Jamhuri imeweka mapingamizi dhidi ya maombi yaliyofunguliwa na mwanashabari Saed Kubenea kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, kuomba kibali cha kumfungulia kesi ya matumizi mabaya ya madaraka aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Mapingamizi yaliyowekwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwanza ni madai kwamba Kubenea hana maslahi na maombi hayo.
Wakili wa Kubenea, Hekima Mwasipu amesema kuwa mapingamizi mengine yaliyowekwa ni kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kuyasikiliza, na sheria iliyotumika kuyafungua haikuwa na nguvu wakati tuhuma za Makonda kuvamia ofisi za Clouds Media Group zinapodaiwa kufanyika.
Pingamizi la mwisho ni kuwa maombi hayo yalitokana na habari za kusikia.
Makonda anadaiwa kuwa Machi 17, 2017, akiwa na watu waliobeba silaha za moto, alivamia ofisi hizo na kuingilia urushaji wa matangazo ya televisheni.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo ya Kubenea, anadai kitendo cha Makonda kuvamia kituo cha televisheni, tena akiwa ameongozana na askari waliobeba silaha za moto, ni kinyume cha Sheriaya Kielektroniki na Posta ya Mwaka 2010.