
Marekani imetangaza kupunguza msaada wa dola za Marekani milioni 50 [TZS bilioni 134.3] kwa sekta ya afya nchini Zambia, kutokana na nchi hiyo kushindwa kushughulikia wizi wa dawa na vifaa tiba vilivyotolewa na Marekani.
Balozi wa Marekani nchini Zambia, Michael Gonzales amesema uamuzi huo umekuja kufuatia onyo la mara kwa mara kwa nchi hiyo, na kwamba Marekani haiko tayari kuwanufaisha mafisadi.
“Hatuko tayari tena kukubali kunufaisha walaghai au mafisadi wakati wagonjwa wanakosa au kununua dawa za kuokoa maisha ambazo tumetoa bure,” amesema Balozi Gonzales.
Zaidi ya maduka ya dawa 2,000 kote nchini Zambia yalipatikana yakiuza dawa na vifaa tiba vilivyotolewa na Marekani katika uchunguzi wa mwaka mzima uliofanywa na ubalozi wa Marekani.